CUF YAFUNGA PAZIA LA WAGOMBEA UBUNGE, UDIWANI


Chama cha Wananchi (CUF) jana kilihitimisha zoezi la uchukuaji fomu za kuwania ubunge na udiwani.

Akizungumzia zoezi hilo, Msemaji wa Chama hicho, Abdul Kambaya alisema mwisho wa kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea nyadhifa za udiwani na ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 lilikamilika jana saa kumi jioni kwa nchi nzima.
Alisema hatua itakayoendelea ni kupitia maombi hayo ili kuwapata watakaopitishwa kuwania nafasi walizoziomba.
“Uchukuaji fomu kwa wagombea wa ubunge na udiwani  umekamilika. Baada ya hapo hatua itakayofuata itakuwa ni kuchambua maombi hayo ili kupata wagombea watakaokiwakilisha chama katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu” alisema Kambaya.
Alisema kuwa, “ni mapema sana kujua idadi ya waliojitokeza kuchukua fomu hadi takwimu zipatikane kutoka maeneo yote ya nchi ndipo ijulikane ni wagombea wangapi wamechukua fomu za kuwania ubunge au madiwani”.
CUF ni moja  ya vyama vinavyounda  kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ambapo vingine ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi  na NLD.  Vyama hivyo vingine bado havijaanza kutoa  fomu kwa wagombea wa ubunge na udiwani.

No comments: