Ndugu
wawili akiwemo mwanamke mwenye ujauzito wa miezi saba, wamefariki dunia katika
kijiji cha Zege kata ya Dindira wilayani Korogwe, wamekufa papo hapo na wengine
wawili kujeruhiwa vibaya baada ya kuangukiwa na mti wakati wakitafuta kuni
msituni.
Waliokufa
kutokana na kuangukiwa na mti aina ya msambu ni Mariam Saidi (17), mwanafunzi
wa kidato cha nne katika Sekondari ya Dindira na Selina Saidi (29) aliyekuwa
mjamzito.
Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki alithibitisha kifo hicho na kusema
kilitokea mwishoni mwa wiki wakati wanawake wane, ambao ni ndugu wa familia
moja walipokuwa wakikata kuni kwenye msitu wa Sakale, jirani na kijiji chao.
Alitaja
waliojeruhiwa kwenye tukio hilo kuwa ni Zubeda Seif (19) na Batuli Saidi (15),
ambaye naye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Dindira.
“Siku
hiyo ya tukio wanawake hao wanne waliingia msitu wa Sakale kwa lengo la kukata
kuni na wakati wakiendelea na shughuli hiyo bila kujua kumbe walikuwa chini ya
mti mkubwa wa Msambu ambao ulikuwa umeshakauka siku nyingi,” alisema.
Alisema
uchunguzi wa awali, umeonesha kuwa mizizi ya mti huo, ilishakauka siku nyingi
na kufikia hatua ya kulegea, kiasi cha kuyumba na kuwaangukia wakati huo
walipokuwa wakiendelea kukata kuni chini yake.
“Inaonyesha
tukio la kuanguka kwa mti huo, lilikuwa la ghafla sana na hivyo kusababisha
Selina na Mariam kushindwa kukimbia ili kujinusuru, hasa baada ya miili yao
kufunikwa kabisa na mti huo”, alisema.
Aliongeza
“Kitendo hicho kilisababisha Mariam kupasuka kichwa papo hapo na Selina ambaye
alikuwa mjamzito naye kupoteza maisha yake na ya mtoto tumboni…kwa bahati
Zubeda na Batuli wao walifanikiwa kukimbia lakini matawi ya mti huo yaliwapiga
na kuwajeruhiwa maeneo tofauti tofauti ya mwili,” alisema.
Hata
hivyo, Ndaki alisema majeruhi hao wamelazwa katika Kituo cha Afya cha Bungu kwa
matibabu na kwamba hivi sasa hali ya afya zao zinaendelea vizuri.
*Picha ya Maktaba.
No comments:
Post a Comment