BABA WA MTOTO ALBINO, WAGANGA 10 WATIWA MBARONI


Polisi mkoani Rukwa inawashikilia watu 17 wakiwemo waganga wa jadi 10 wakihusishwa na tukio la kikatili  katika kijijini cha Kipeta, Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga  ambako mtoto mlemavu  wa ngozi (albino), Baraka Cosmas mwenye umri wa miaka 6 (pichani) mwishoni mwa wiki  alishambuliwa na kukatwa kiganja  cha mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana.

Miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa ni watu saba ambao wanatuhumiwa kushiriki katika kumkata kiganja mtoto huyo mlemavu wa ngozi akiwemo baba yake, mzazi Cosmas Yoram (32).
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Ferdinand Rwegasira amethibitisha kukamatwa kwa  watuhumiwa hao  kufuatia  msako  mkali  uliofanyika katika  vijiji  vinne vya wilaya za Sumbawanga na Nkasi.
Aliwataja waliokamatwa  pamoja na baba mzazi wa mtoto  huyo  kuwa ni pamoja na Mwendesha William (30), Masunga Bakari (50), na Ngolo Masingija (47) wote kutoka kijiji cha Kaoze .
Wengine ni Paschal Jason (40), David Kiyenze (45) na Mageta Shimba (46), wote wakazi wa  kikiji cha Kipeta , Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga.
Kwa mujibu wa Rwegasira, katika msako huo  pia  walikamatwa waganga wapiga ramli chonganishi 10 akiwemo Sererino Kachingwe “Nakalango”(70), mkazi wa kijiji  cha Miangalua  wilayani  humo  ambaye pia  alipatikana na  bunduki aina ya Shot gun  greener  yenye  namba G 73354 TZD,CAR 47478 ambayo anaimiliki isivyo  halali .
“Mtuhumiwa huyu  pia ni mganga wa kienyeji  ambapo  alikutwa  na wanyama wawili aina ya Kalunguyeye  wakiwa hai  pamoja na dawa mbalimbali za miti  shamba. Pia katika msako  huo amekamatwa mganga mwingine wa kienyeji , Eliza Malongo  mwenye umri wa miaka 36 mkazi wa kijiji cha Kamnyalila  akiwa na nyara za Serikali, “ alieleza.
Aliongeza Eliza alikutwa na ngozi ya chui, wanyama wanne waliokaushwa aina ya Kalunguyeye na nywele zinazodhaniwa kuwa za binadamu pamoja na mfupa wa swala.
Waganga wengine waliokamatwa katika msako huo ni pamoja na Sodeli Malimbo ‘Chuchi” (69) mkazi wa kijiji cha Miangalua, Akobo Chinzwe (50), Leonard Samson (59) na Engelbert Kasinde (45) , wote wakazi wa kijiji cha Kamyalila.
Katika orodha hiyo  wapo Boniface Chalya (49)  na Julius Simbamwene (40) wote wakiwa wakazi wa kijiji cha Mpui .
“Watuhumiwa hawa  walikutwa na  vifaa mbalimbali  vya kupigia ramli  vikiwemo  vioo  viwili, pembe moja, ndege na wanyama  ambao  hawakuweza kutambulika mara moja, mizizi ya aina mbalimbali  na dawa  mbalimbali za kienyeji,“ alieleza Rwegasira.
Akifafanua zaidi, Rwegasira alidai kuwa msako huo pia ulifanyika wilayani Nkasi ambako  alitiwa nguvuni mganga  wa kienyeji  aitwae Charles Misalaba (47) , mkazi wa kijiji cha Kacheche  ambapo  alikutwa na yai la mbuni ,  kucha za chui , pembe ya korongo , ngozi ya paka pori  na kobe aliyekaushwa.
Amesisitiza kuwa msako  huo  bado unaendelea na kwamba  watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani  mara tu baada ya upelelezi wa awali wa shauri lao  kukamilika
Kwa mujibu wake msako huo unafuatia watu wasiojulikana  kumshambulia  na kumkata kiganja mtoto mwenye umri wa miaka sita, Baraka Cosmas na kisha kutokomea nacho kusikojulikana usiku wa kuamkia Machi 08, mwaka huu.
Tukio hilo lililotokea katika kijiji cha Kipeta Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga, ambako mtoto huyo anaishi na wazazi wake, Cosmas Yoram (32) na Prisca Shaaban pamoja  na watoto  wengine wawili  ambao nao  ni albino  wakiwa na umri wa miaka nane na minne.
Alisema tukio hilo ni la saa nane  usiku wa kuamkia Jumapili wakati mtoto huyo akiwa amelala na mama yake. Baba wa mtoto huyo hakuwepo wakati huo.
Akielezea zaidi, Kaimu Kamanda Rwegasira  alisema usiku huo kikundi cha watu wasiojulikana walivamia nyumba alimolala Baraka na mama yake mzazi, Prisca wakiwa na silaha za jadi, ikiwemo mapanga na fimbo na kuanza kumshambulia kwa kumcharaza viboko Prisca baada ya kukataa kuwapatia mtoto huyo, mwenye ulemavu wa ngozi.
“Baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo walimwamuru mama mzazi wa mtoto Baraka kuwakabidhi mtoto huyo, lakini alikaidi ndipo walipoanza kumshambulia kwa kumpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kumjeruhi vibaya … “Waliingia ndani baada ya kuvunja mlango wa nyumba hiyo, ndipo katika patashika hiyo wavamizi hao walimkata mtoto Baraka kiganja cha mkono wake wa kulia na kuondoka nacho kusikojulikana,” alibainisha.
Aliongeza kuwa wakati hayo yakitokea, baba mzazi wa mtoto huyo inadaiwa alikuwa amelala katika nyumba ya mkewe mdogo kijijini humo.
Kwa mujibu wa Rwegasira , mtoto huyo na mama yake  walikimbizwa   katika Kituo cha Afya cha Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya ambapo walipewa  huduma ya kwanza  kisha  wakahamishiwa Hospitali ya wilaya ya Mbozi  ambapo  baadaye kuhamishiwa katika Hospitali ya Rufaa jijini Mbeya kwa matibabu zaidi.

No comments: