HIVI NDIVYO ZITTO ALIVYOTIMULIWA CHADEMA NA KUVULIWA UBUNGE


Hatima ya ubunge wa Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), sasa iko njia panda.

Hali hiyo inatokana na hatua ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam  kutupilia mbali kesi ya madai iliyofunguliwa na Mbunge huyo dhidi ya chama chake.
Jaji Richard Mziray alitupilia mbali kesi hiyo jana baada ya kukubali pingamizi la awali lililowasilishwa na Chadema kupitia mawakili wake Peter Kibatala, Tundu Lissu na John Mallya ambao walidai kesi hiyo ilifunguliwa bila kufuata utaratibu wa sheria.
Zitto ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, alifungua kesi hiyo dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya Chadema na Katibu Mkuu wake, akiiomba Mahakama ikizuie chama kujadili uanachama wake, hadi rufaa anayokusudia kuikata Baraza Kuu la chama kupinga kuvuliwa nyadhifa, itakaposikilizwa.
Akitoa uamuzi huo Jaji Mziray alikubali hoja mbili kati ya tano zilizokuwa zimewasilishwa na Chadema na kumtaka Zitto kulipa gharama za uendeshaji wa kesi hiyo .Aidha alisema Chama kinaweza kuendelea na taratibu zake kama jinsi zilivyokuwa zikiendelea kabla ya kuwekwa zuio.
Kabla ya kusikilizwa kwa kesi hiyo, Januari mwaka jana, Mahakama  ilitoa zuio la muda kwa Chadema kutojadili suala lolote la uanachama wa Zitto hadi kesi ya
Msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Katika kesi hiyo namba 1 ya 2014, Zitto aliiomba mahakama hiyo imwamuru Katibu Mkuu wa Chadema ampatie mwenendo na taarifa za Kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kilichomvua nyadhifa zote alizokuwa nazo ndani ya chama na iwazuie walalamikiwa kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu yake kama Mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Katika hoja zao za pingamizi Chadema walidai, kesi hiyo haina msingi kwa sababu haikuwasilishwa katika Mahakama ya chini kusikilizwa na kutolewa maamuzi kwa mujibu wa kifungu cha 13 cha Mwenendo wa Kesi za Madai.
Walidai kesi hiyo imewasilishwa masijala Kuu ya Mahakama Kuu badala ya masijala ya Wilaya kinyume cha sheria na taratibu za masijala za Mahakama pia Zitto hajaomba maoni ya Mahakama Kuu kuhusiana na suala linalohusiana na uanachama wake Chadema.
Aidha, walidai shauri hilo halina msingi kisheria kwa kuwa Zitto anaendesha mashauri mawili, Mahakama Kuu na rufaa ya kwenye Baraza Kuu la chama pia Mahakama Kuu siyo mahali pake kwa sababu Zitto hajatumia nafasi zilizopo ndani ya Chadema.
Mahakama Kuu haina mamlaka ya kutoa uamuzi wa kuzuia Zitto asijadiliwe uanachama wake kwa sababu ni kwa kufanya hivyo itakuwa inaingilia mamlaka ya Chama katika kuwaadhibu wanachama wake.
Kesi hiyo ilifunguliwa Januari mwaka jana na kuanza kusikilizwa mbele ya Jaji John Utamwa.
Akizungumzia hukumu hiyo inayouweka ubunge wake njiapanda endapo chama chake kitaamua kumuengua kama ilivyokuwa kwa washirika wake wa kisiasa, Profesa Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba waliojiunga na chama kipya cha ACT, Zitto alisema yeye na wakili wake hawakuwa na taarifa juu ya hukumu hiyo.
Aidha, Tundu Lissu ambaye ni Mkurugenzi wa Sheria wa Chadema na Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema: "Kwa mujibu wa katiba ya Chadema, mwanachama yeyote anapofungua kesi mahakamani dhidi ya chama chake, endapo atashindwa katika kesi hiyo atakuwa amejiondoa uanachama wake, kwa hiyo natangaza rasmi Zitto Kabwe sio mwanachama tena wa Chadema.
Akiwa katika ofisi za makao makuu ya Chadema, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Lissu alisema ni wazi baada ya mbunge huyo kushindwa kesi iliyokuwa imefunguliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, sasa amefutwa uanachama.
“Kwa mujibu wa taratibu na sheria ya chama isemayo  kwamba endapo mwanachama atapata tatizo lolote binafsi ama la kichama, malalamiko yote yatasuluhishwa ndani ya chama na si mahakamani.
“Hivyo,  kwa mujibu wa sheria za chama, Zitto alikiuka sheria  anapaswa kuvuliwa uanachama wake,” alisema Lissu.
Lissu aliongeza kuwa hata kama Zitto angeweza kwenda kushitaki lazima angeanzia katika mahakama ndogo za wilaya yaani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi au Masijala ya Mahakama ya Wilaya tofauti na alivyopeleka kesi hiyo moja kwa moja Mahakama Kuu.
Aliongeza kuwa, kutokana na Mahakama kumtaka Zitto kukilipa chama chake gharama zote za kesi hiyo, Chadema itakaa na kutathmini gharama husika.
Kuhusu utambulisho wa Zitto bungeni, Lissu alisema  kwa mujibu wa kanuni za chama chake, Katibu wa chama chake anatakiwa kumwandikia barua Mwenyekiti au Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi kumjulisha  Zitto tena si mwanachama wao na taratibu zingine zitafuata.

No comments: