MTUHUMIWA FEDHA ZA ESCROW AJIKOROGA


Mkurugenzi Mdhibiti Uchumi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Dk James Diu, amejichanganya mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, kuhusu matumizi halisi ya fedha alizozipokea kutoka kwa James Rugemalira ambazo ni Sh milioni 80.8.

Akijitetea mbele ya baraza hilo, Mkurugenzi huyo ambaye pia aliwahi kushika wadhifa wa Meneja Udhibiti Uchumi katika Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), alikiri kupokea kiasi hicho cha fedha ambacho alidai alikitumia kwa ajili ya matibabu ya mkewe aliyefariki dunia Agosti mwaka jana kwa ugonjwa wa saratani.
Hata hivyo, katika maelezo yake aliyoyatoa mbele ya Kamati ya Uchunguzi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na tamko lake la mali na madeni alilolitoa Desemba 30, mwaka jana katika Sekretarieti hiyo, kiongozi huyo alibainisha kutumia kiasi hicho cha fedha katika kulipia deni lake la nyumba alilokuwa akidaiwa.
Awali Wakili wa Sekretarieti hiyo ya maadili, Wemaeli Mtei, akimsomea mashtaka mkurugenzi huyo, alidai kuwa mlalamikiwa huyo anadaiwa kuomba na kupokea Sh milioni 80.8 kutoka kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited kinyume cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Alisema pamoja na fedha hizo, pia mlalamikiwa huyo anadaiwa kujipatia maslahi ya kiuchumi kwa kupokea kiasi cha dola za Marekani 25,000 kutoka kampuni ya Mabibo Beers, Wine and Spirit mali ya Rugemalira, kinyume cha Sheria hiyo ya maadili, inayokataza kiongozi wa umma kuomba na kupokea maslahi binafsi.
Aidha katika hati hiyo ya mashtaka mlalamikiwa huyo pia anadaiwa kupokea dola za Marekani 10,100 kutoka Kampuni ya Prime Fuel Tanzania Limited ambazo zote hakuzitamka kama Sheria hiyo ya maadili inavyotaka.
“Mlalamikiwa ambaye pia kuanzia mwaka 2006 hadi 2011 aliwahi kufanyakazi katika taasisi ya Serikali ya Ewura inayoshughulika na masuala ya nishati, alijipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kampuni ya VIP yenye hisa asilimia 30 na kampuni ya IPTL yenye mkataba wa umeme na Tanesco, jambo linalosababisha mgongano wa kimaslahi,” alisema Mtei.
Shahidi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Zahara Guga, alisema kitendo cha mlalakiwa kuwa na historia ya kufanya kazi EWURA na kupokea fedha kutoka kampuni ya VIP ambayo inasimamiwa na mamlaka hiyo ni kinyume na Sheria ya maadili na pia mgongano wa kimaslahi.
Alisema katika uchunguzi wa kamati hiyo ya uchunguzi, walibaini kuwa mlalamikiwa alifungua akaunti Februari 4, mwaka jana na kuingiziwa Sh milioni 80.8 Februari 5, mwaka huo na kampuni ya VIP katika akaunti yake iliyopo benki ya Mkombozi tawi la Kariakoo.
Akijitetea mbele ya baraza hilo, Dk Diu, alikanusha kuomba fedha hizo kwa Rugemalira na kukiri kuwa alipokea kiasi hicho cha fedha ambazo alipatiwa kama ahadi ya kumsaidia katika matibabu ya mkewe, ikiwa ni pamoja na kumsafirisha kwenda India kwa matibabu zaidi.
“Rugemalira  ni rafiki yangu wa karibu pamoja na familia yangu, lakini pia nimesoma naye wakati natafuta shahada yangu ya kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1982 hadi 1985, alinipatia fedha hizi kama ahadi sijamuomba, kudai wala kupokea maslahi ya kiuchumi kutoka kwake,” alisisitiza.
Alisema kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo mkewe, Rugemalira alikwenda kumjulia hali alipolazwa hospitali ya TMJ na baadaye Sanitarius iliyopo Mikocheni ndipo alipoahidi kutoa fedha hiyo kama mchango na msaada wa matibabu na baadaye mazishi baada ya mkewe huyo kufariki dunia.
Aidha alisema hata katika fomu yake ya tamko la mali na madeni kwa sekretarieti hiyo, aliyoiwasilisha Februari 30, mwaka jana aliitamka fedha hizo kuwa ameipokea kutoka kwa Rugemalira. “Awali sikuona umuhimu wa kuiwasilisha kwa ofisa masuhuli wangu kwa sababu haikuwa zawadi na sikuona umuhimu wa kufanya hivyo,”
Aidha alisisitiza kuwa kupokea kwake fedha hizo hakuna mgongano wowote wa kimaslahi kwa kuwa hana uhusiano wowote wa kibiashara na Rugemalira na hata kazi yake katika mamlaka ya TCAA haina uhusiano na kampuni za Rugemalira kibishara.
Hata hivyo, baadaye akionesha maelezo ya Dk Diu mbele ya kamati ya uchunguzi alipohojiwa kuhusu kupokea fedha hizo, Wakili wa Sekretarieti hiyo ya Maadili Getrude Cyriacus, alibainisha kuwa mlalamikiwa huyo alijitetea kuwa fedha hizo alizitumia kulipia deni la nyumba alilokuwa akidaiwa.
“Hata katika tamko la mali na madeni aliloliwasilisha mwaka 2012, aliandika maelezo kuwa anadaiwa Sh milioni 80 za nyumba ambayo haijakamilika aliyonunua huko Mbezi kutoka kwa Godson Shangwe, na tamko lake la mwaka jana alibainiha kuwa ametumia fedha hizo alizopewa na Rugemalira kumalizia deni hilo,” alisema Cyriacus.
Baada ya kubanwa na hoja hiyo, alijitetea mbele ya baraza hilo, kuwa ni kweli alitumia Sh milioni 80.8 kulipia deni hilo la nyumba kutoka kwa Rugemalira lakini fedha hizo si hizo zinazodaiwa na Sekretarieti bali ni nyingine.
Aidha wakili huyo alibainisha kuwa kwa mujibu taarifa ya benki ya mteja aliyowasilisha mbele ya baraza hilo, ilionesha kuwa mlalamikiwa aliwekewa fedha hizo Februari 5, mwaka jana, na Februari 8, mwaka huo alitoa Sh milioni 40, Februari 10 akatoa milioni 35 na hadi kufikia Machi 15 alishatoa jumla ya Sh milioni 70.
“Sasa umetuambia hapa fedha hizo umetumia kumtibia mkeo na kwamba mmesafiri kwenda India Agosti mwaka jana hadi kifo cha mkeo, sasa mbona taarifa hizo za benki zinaonesha umetoa fedha hizo takribani zote Machi, mwaka huo na pia umekiri kulipia nyumba, lipi sasa umelifanyia kwa fedha hii?,'' alihoji.
Katika kujitetea zaidi alibainisha kuwa fedha hizo alizopokea kwa Rugemalira hazikuwa zawadi au msaada bali mkopo wenye masharti nafuu ambao hajapewa muda wa kulipa, lakini pia alishindwa kuwasilisha vielelezo vya mkataba wa mkopo huo. “Ilikuwa ni mkataba wa mdomo, sina ushahidi hapa,”
Cyriacus, akihitimisha hoja hiyo, alisema mlalamikiwa anastahili kujibu mashtaka na kutoa maelezo zaidi, kwa kuwa amejichanganya kuhusu matumizi ya fedha alizopatiwa huku akishindwa kuwasilisha vielelezo vya fedha hizo kuwa mkopo.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Jaji Hamisi Msumi, alisema kuwa imesikiliza shauri hilo na litatoa uamuzi wake na mapendekezo kwa mamlaka husika.

No comments: