MOTO WACHOMA MAKAZI YA WACHIMBAJI 3,500 MIRERANI


Moto mkubwa uliozuka usiku wa kuamkia jana katika machimbo ya madini ya tanzanite yaliyopo Mirerani, Simanjiro mkoani Manyara, umeteketeza kabisa makambi ya migodi 17, ikiwemo mitambo ya uchimbaji, na kusababisha wachimbaji zaidi ya 3,500 kukosa makazi, huku ajira zao sasa zikiwa shakani.

Mwandishi alipotembelea eneo hilo jana, lilikutana na sura za simanzi za vijana hao waliosema moto huo ulisababishwa na hitilafu ya umeme.
Kutokana na tukio hilo, wachimbaji hao waliokuwa wameajiriwa na wamiliki wa migodi hiyo, walisema kwao hilo ni janga kama yalivyo majanga mengine na kwamba, kwa sasa hawajui la kufanya na hivyo kuiomba serikali kuangalia namna ya kuwasaidia katika muda mfupi ambao wakisubiri kujua hatima yao ya kazi.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari katika eneo la tukio, moto huo ulioanza kuunguza nyumba hizo majira ya saa 9.30 alfajiri uliteketeza mashine za uchimbaji, mashine za kuingiza hewa, jenereta za umeme, mota za pampu, na waya za umeme na vifaa mbalimbali vya uchimbaji vyenye thamani ya mabilioni ya fedha.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mahmoud Kambona aliyetembelea eneo hilo jana,  alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya transfoma ya umeme iliyokuwa ikitengenezwa na mafundi wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) na hasara aliyoiona inaweza kuwa kubwa sana lakini hawezi kusema kwa sasa.
Kambona alisema kutokana na hali hiyo kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Simanjiro itakaa na kuchunguza kwa kina na kutoa taarifa rasmi ya hasara iliyopatikana kutoka na moto huo.
Hata hivyo, Mkuu huyo alisitikitishwa na hali aliyoikuta ya mji wa Mirerani na Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro kutokuwa na gari la zimamoto katika migodi hiyo hatua ambayo alisema hawezi kuiacha kwani ni lazima gari la zimamoto liwepo katika eneo la migodi kwa usalama zaidi.
Alisema kwa sasa wilaya itakaa na kutoa ushauri kwa wamiliki wa migodi hiyo namna ya kuwasaidia vijana waliokuwa wakifanya kazi katika migodi yao katika muda ambao hawatakuwa na kazi.
‘’Hapa kuna mambo mawili moja eneo la mgodi kutokuwa na gari la zimamoto hilo lazima lishughulikiwe haraka na uongozi wa halmashauri  na mji wa Mirerani.
‘’Pili vijana zaidi ya 3,500 hawana ajira hivyo ni lazima hatua za dharura zinapaswa kuchukuliwa na wamiliki wa migodi na serikali nini cha kufanya juu ya hali hiyo,’’ alisema Kambona.
Mmoja wa wachimbaji wadogo wa Kitalu B aliyejitambulisha kwa jina la
Africanus Mbuya, alisema chanzo cha moto ni hitilafu ya umeme iliyotokea katika nguzo ya umeme ambayo ilikuwa ikitengenezwa na mafundi wa Tanesco wa mji wa Mirerani na kudai kuwa mafundi wa shirika hilo ni tatizo.
Alisema mara baada ya kutokea hitilafu hiyo, ghafla moto ulianza kulipuka katika nyumba ya mgodi wa Loika na kuanza kusambaa kwa kasi sana katika nyaya za umeme na kwenye jenereta na mashine zingine kunasa, lakini mafundi hao waliamua kukimbia bila kuchukua hatua za kuzima moto huo.
Naye Juma Abdallah, alisema wamechanganyikiwa kutokana na hasara waliyoipata, hivyo kuiomba Serikali kuangalia jinsi ya kuwasaidia wachimbaji hao.
Aidha, kwa upande vijana hao waliokuwa wameajiriwa kwa ajili ya uchimbaji, wakizungumza kwa hisia kali walisema kwa sasa hawajui cha kufanya, kwani kwa jinsi hali ilivyo ni dhahiri watakaa bila ya kufanya kazi kwa muda fulani.
“Ni balaa kwetu. Pamoja na hasara ya vitu vyetu na mali za matajiri, ni wazi kwamba hapa sasa hakuna kazi…tunarudi kwenye maisha yale yale ya kutangatanga. Tunamuomba Mungu ashushe baraka zake ili tuendelee na kazi,” alisema mmoja wa wachimbaji hao, Alfred Shao 'Rasta’.

No comments: