Wakazi
10 wa jijini hapa, akiwemo mwanafunzi wa sekondari wamefikishwa mbele ya
Mahakama ya Hakimu Mkazi wakikabiliwa na makosa matano tofauti kuhusu tukio la
kuwanyang’anya polisi silaha pamoja na kumuua
askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Sajenti Mohamed
Rashid Kajembe.
Mwanafunzi
aliyefikishwa mahakamani ni Rajab Bakari (19) ambaye ni mwanafunzi wa shule ya
sekondari na mkazi wa Makorora jijini hapa.
Watuhumiwa
tisa wameelezwa kuwa ni wafanyabiashara, nao ni Mbega Seif (25) maarufu 'Abuu
Rajab' mkazi wa Kiomoni, Amboni, Ayubu Ramadhani (27) maarufu 'Chiti' ambaye ni
fundi umeme na mkazi wa Kona Z Kiomoni, Hassani Mbogo (20) maarufu 'Mpalestina'
mkazi wa Makorora, Mohamed Ramadhani
(19) mfanyabiashara na mkazi wa Makorora, Sadiki Mdoe (25) maarufu 'Kizota au
Kisaka' mkazi Magaoni.
Washtakiwa
wengine ni Saidi Omari (26) mkazi
wa Magaoni Tairi Tatu, Nurdin Mbogo (27)
Makorora, Ramadhan Mohamed (18) mkazi wa
Donge pamoja na Omari Harubu Abdala (55) maarufu 'Ami' mkazi wa Dunia
Hoteli Makorora.
Wakisomewa
mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Aziza Rutala, Wakili wa Serikali, George
Barasa akisaidiana na MariaClara Mtengule, walidai kuwa kosa la kwanza hadi la
tatu linawahusisha washitakiwa namba moja mpaka nane (1 -8) ambao wanatuhumiwa
kushiriki kula njama ya kutenda kosa
kinyume cha sheria.
Barasa
alidai kuwa katika maeneo tofauti ya jijini Tanga kati ya Septemba mosi
2014 hadi Januari 26 mwaka huu,
washitakiwa wote wanane kwa pamoja walitenda kosa la kula njama na kufanya kosa
la unyang’anyi wa silaha.
Katika
kosa la pili, Barasa alidai mahakamani
hapo kwamba mnamo Januari 26 mwaka huu, katika mgahawa wa Jamali ulipo kati ya
barabara ya Nne na ya Tano jijini Tanga, washitakiwa wote wanane waliiba silaha
moja aina ya SMG namba za usajili
14303545 mali ya Polisi na muda mfupi
kabla ya kutenda kosa hilo walitumia visu kumchoma askari H 501 Mwalimu ili
kupata silaha hiyo.
Kosa la
tatu la washitakiwa hao ni unyang’anyi wa kutumia silaha, na washitakiwa wote
wanane wanadaiwa kuwa katika mgahawa wa
Jamali uliopo kati ya barabara ya nne na ya tano waliiba silaha nyingine yenye
namba za usajili 14301230 SMG mali ya
polisi na kwamba muda mfupi kabla ya kutenda kosa hilo walimtishia kwa
kutumia nguvu kumnyang’anya silaha PC H Mansoor kinyume na sheria.
Hata
hivyo, katika kosa la nne ambalo limemhusisha mshitakiwa namba tisa Nurdin
Mbogo wakili huyo wa Serikali, alidai kuwa Februari 6 mwaka huu, katika sehemu
isiyofahamika jijini Tanga, mshtakiwa huyo akijua kuwa Hassan Mbogo (Mshitakiwa
Na. 4) alitenda kosa Septemba mosi 2014 na Januari 26 mwaka huu alimsaidia
kumwezesha kukwepa kushtakiwa na kuadhibiwa kinyume na sheria.
Katika
hatua nyingine, Wakili wa Serikali Mtengule alisoma shitaka jingine jipya
ambalo
liliwahusisha watuhumiwa watatu akiwemo namba 1 na 2 (Mbega Rajabu na Rajabu
Bakari) pamoja na mshtakiwa mwingine Omari Harub Abdallah 'Ami' wakidaiwa kwa
pamoja kuhusika kumuua askari wa JWTZ,
Sajenti Mohamed Rashid Kajembe mnamo Februari 13 mwaka huu katika Mapango ya Amboni Jijini Tanga kinyume
cha sheria namba 196 na 197 ya makosa ya adhabu ya mwaka 2002 .
Washtakiwa
hao watatu hawakutakiwa kujibu lolote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na
uwezo wa kusikiliza kesi hiyo ya mauaji.
Hata
hivyo, washitakiwa wote 10 kwa pamoja
wamekana makosa yao, na mahakama imewanyima dhamana washitakiwa tisa kutokana
na makosa waliyotenda kutokuwa na
dhamana.
Mshitakiwa
namba tisa Nurdin Mbogo alishindwa kutimiza masharti ya dhamana baada ya
kutakiwa kutoa Sh milioni moja na mdhamini mmoja mwenye mali isiyohamishika
yenye thamani ya Sh milioni moja.
Washitakiwa
wote wamerudishwa rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Machi 23 mwaka huu
kwa kuwa upelelezi wake haujakamilika.
Mnamo
Februari 13 mwaka huu katika eneo la Amboni Jijini Tanga palizuka mapigano
baina ya askari polisi wakishirikiana na JWTZ dhidi ya watu wanaodaiwa kuwa ni
majambazi, waliokuwa wamejificha kwenye mapango ya Majimoto.
Katika
tafrani hiyo, kulisababish kifo cha askari wa JWTZ na majeruhi watano wakiwemo
wanajeshi wawili na Polisi watatu, hali iliyozua hamaki kwa wakazi wa jijini
hapa.
Rais
Jakaya Kikwete katika hotuba yake mwezi uliopita alielezea matukio hayo kuwa ni
ya ujambazi, lakini pia yana mwelekeo wa ugaidi na akalitaka jeshi la polisi kuwasaka watuhumiwa wote na kuwafikisha
kwenye vyombo vya sheria.
No comments:
Post a Comment