MTOTO ALBINO ANUSURIKA KUUAWA NA WAWINDAJI MPIRANI


Mtoto wa umri wa miaka sita, mwenye ulemavu wa ngozi (albino), anayeishi Kijiji cha Ndoleleji, amekoswakoswa na watu waliokuwa wakimvizia akiwa katika michezo, baada ya watoto wenzake kuchukua uamuzi wa kumlinda.

Taarifa zilizomfikia mwandishi, zilieleza kuwa ‘wawindaji’ hao waliokuwa na gari lililokuwa na vioo vya giza, walionekana wakimfuatilia mtoto huyo Jumamosi ya wiki iliyopita alipokuwa akiogelea mtoni na baada ya kumkosa, wakamfuatilia katika uwanja wa mpira Jumatatu, ambako nako walimkosa.
Akizungumza na mwandishi, diwani wa Kata ya Shagihilu wilayani Kishapu mkoani hapa, Mohamed Amani alisema  kumefanyika majaribio mawili ya kutaka kumteka mtoto huyo (jina limehifadhiwa), lakini kwa msaada wa watoto wenzake hayakufanikiwa.
Kwa mujibu wa Diwani Amani, Jumamosi iliyopita watu watatu wakiwa kwenye gari hilo, walifika kijijini hapo na kwenda mpaka mtoni, ambako mto huyo mwenye ulemavu wa ngozi alikuwa akicheza na wenzake.
Baada ya kufika mtoni, watu hao wote watatu waliteremka kwenye gari na kusogea katika eneo la mto, hatua iliyowashitua watoto wenzake waliokuwa wakicheza wote mtoni.
Kwa mujibu wa Amani, watoto hao wenye umri mkubwa zaidi ya mtoto huyo, walitambua hatari iliyokuwa ikimkabili mwenzao mwenye ulemavu wa ngozi na
dalili za watu hao waliokuwa hawawafahamu, waliokuwa wakizidi kuwasogelea.
Baada ya kuona watu hao wakizidi kusogelea eneo lao la michezo, watoto hao walimshauri mwenzao mwenye ulemavu wa ngozi, akimbilie nyumbani kwao na mtoto huyo akasikia ushauri huo na kurudi nyumbani.
“Baada ya mtoto (albino) kukimbilia nyumbani kwao, wale watu waliingia kwenye lile gari na kuondoka,” alisema Amani na kuongeza kuwa hatua ya watu hao kutosema lolote kwa watoto hao lilizidi kuwapa mashaka.
Jumatatu ya wiki hii jioni wakati mtoto huyo alipokuwa na wenzake, wakiwemo wale aliokuwa nao mtoni, wakicheza mpira wa miguu katika kiwanja cha kijijini hapo, gari hilo lililoonekana mtoni, lilifika uwanjani hapo na kusimama.
Inaelezwa kuwa baada ya kusimama, watu wale watatu walioonekana mtoni walishuka katika gari hilo, wakaegemea gari na kuangalia watoto hao wakicheza mpira, akiwemo mwenzao mwenye ulemavu wa ngozi.
“Safari hii haikuwa mtoni, bali katika eneo jingine tena la wazi ambalo mtoto huyo alikuwa akicheza mpira na wenzake… walipofika walisimama nje ya gari lao,” alisema Diwani Amani.
Kutokana na hali hiyo, watoto hao walihisi kuna hali ya hatari kwa mwenzao, baada ya watoto hao kuona gari hilo kwa mara nyingine, na watu hao wakiwa wamewasimamia na hawakuwa wakizungumza chochote.
Diwani huyo alisema watoto hao walisitisha mchezo wao, na kumtaka mwenzao kwa mara nyingine akimbilie nyumbani kwao, ili kusalimisha maisha yake kutokana na utata wa usalama ulioanza kujitokeza hapo.
Akizungumza na mwandishi, mama mzazi wa mtoto huyo, Regina Malando, alithibitisha kurejea nyumbani mara mbili kwa mtoto wake huku akikimbia.
Regina alisema baada ya kurejea nyumbani, mtoto huyo alimweleza kuwa kuna watu asiowafahamu waliokuwa wamesimama kando ya uwanja waliokuwa wakifanyia mazoezi na kwamba anawaogopa.
Mama huyo alisema, baada ya kupewa taarifa hizo mara mbili, alimsihi mtoto wake aingie ndani na atulie na akome kwenda kucheza mbali na nyumbani kwao na mtoto huyo akatii ushauri wa mama yake.
Baba wa mtoto huyo, Tito Shija, alisema aliposikia taarifa hiyo ya pili, alikwenda katika uwanja huo na kukuta watu hao wakiingia kwenye gari na kuondoka kwa kasi.
Shija alisema kwa bahati mbaya hakuweza
kuchukua namba za usajili wa gari hilo, ila alishuhudia kuwa gari hilo lilikuwa na vioo vya giza sehemu zote.
Kwa mujibu wa Shija, kesho yake binti mmoja ambaye hakumtaja jina, alimwambia kuwa alipita karibu ya hao watu wakamfokea na kumuuliza anatafuta nini huko na
kumwamuru aondoke haraka karibu yao.
Shija alidai kuwa binti huyo alimwambia kuwa wakati akiondoka, alisikia  watu hao wakijadili namna ya kumpata mtoto huyo, wakati alipokuwa akikimbilia kwao.
Diwani Amani alisema, kutokana na hali hiyo alifikisha suala hilo kwenye Kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata na ikaamuliwa mtoto huyo mwenye ulemavu wa ngozi, apelekwe kwenye kituo cha watoto wenye ulemavu wa ngozi, kilichopo Buhangija katika Manispaa ya Shinyanga.                                             
Mwandishi alifuatilia utekelezaji wa uamuzi huo na kuhakikishiwa na Mkuu wa Kituo hicho cha Buhangija, Peter Ajali, kwamba amempokea mtoto huyo na kuongeza kuwa idadi ya watoto katika kituo hicho inaongezeka kila siku, na  sasa wamefikia watoto 349 wenye ulemavu wa ngozi.
Mwanzoni mwa mwezi huu, mtoto mwingine wa kiume mwenye ulemavu wa ngozi, Baraka Cosmas (6) aliyekuwa akiishi na wazazi wake kijijini Kipeta, Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga, alishambuliwa na kujeruhiwa vibaya kwa kukatwa kiganja cha mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana kisha kutokomea nacho kusikojulikana.
Mama mzazi Prisca Shaaban (28), alisema tukio hilo lilimkuta saa saba usiku, wakati akitaka kutoka nje kujisaidia.
“Nilikutana na mtu akifungua mlango, akanipiga ni kitu kichwani kisha nikazimia, nilipozinduka nikapiga kelele na majirani wakafika ndipo nilipogundua mtoto wangu amekatwa kiganja cha mkono wa kulia,” alisema mama mzazi.
*Picha ya maktaba ya mtoto albino aliyekatwa kiganja Rukwa hivi karibuni.

No comments: