MSIBA MZITO WAIKUMBA UDSM, WANAFUNZI WATANO KWA MPIGO WAFARIKI AJALINI

Wanafunzi watano wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ni miongoni mwa watu 50 waliokufa katika ajali ya basi la Majinja, lililogongana na lori katika eneo la Changarawe Mafinga mkoani Iringa.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alisema waliopoteza maisha ni wanafunzi watatu  wa mwaka wa tatu na wawili wa mwaka wa pili, wote kutoka kitivo cha Sayansi ya Jamii (BA Education, COHU).
Alitaja wa mwaka wa tatu kuwa ni Killeo Eric, Sosten Daud na Chiwangu Didimo na wa mwaka wa pili katika kitivo hicho ni Watson Jeremiah na Mbaule Frank aliyekuwa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu Kishiriki cha UDSM cha Elimu cha Dar es Salaam (DUCE).
Alisema miili ya marehemu hao imeshachukuliwa na familia zao na kusafirishwa kwa ajili ya maziko.
Profesa Mukandala alitaja waliojeruhiwa kuwa ni Tupate Mosigwa, ambaye yuko mwaka wa kwanza, ambaye awali alilazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mafinga  na sasa amehamishiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa matibabu zaidi.
Mwanafunzi mwingine aliyejeruhiwa ni Rafael Norbert, aliyekuwa mwaka wa kwanza DUCE, aliyetibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mafinga na kuruhusiwa kurejea nyumbani kwa matibabu zaidi.
Profesa Mukandala alisema uongozi wa chuo hicho unatoa pole kwa familia za wanafunzi hao pamoja na jamii nzima ya UDSM kwa kupoteza wapendwa hao.
Alisema chuo hicho kitaendelea kuwasiliana na mamlaka za Mkoa wa Iringa kufahamu kama kuna majeruhi au marehemu wengine kutoka katika jamii hiyo, na kutaka wanafunzi kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu kwa kuombea familia za wapendwa waliokufa na waliojeruhiwa.
Uongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), pia katika taarifa yake iliyotolewa na Waziri Mkuu wake, Gibson George iliwashukuru wanachuo wote waliokuwa bega kwa bega katika kutambua wenzao.
Alisema  UDSM imepoteza wanachuo wanne na chuo kishiriki cha DUCE, kimepoteza mmoja na kufanya  jumla yao kuwa watano.
Kwa mujibu wa George, utaratibu wa rambirambi unasimamiwa na Serikali ya Wanafunzi katika ngazi ya Shule Kuu, chini ya usimamizi wa wenyeviti na wabunge na mratibu ni  Massawe Chrisostom ambae ni Mwenyekiti wa Kitivo kilichopoteza wanafunzi wanne.
Alisema  kwa niaba ya Daruso wanatoa pole kwa msiba huo na kushukuru uongozi wa chuo kwa kushiriki katika misiba na kuwatuma wawakilishi kutoka chuoni hapo.
Ajali hiyo ilihusisha lori aina ya Scania namba T 689 APJ mali ya Cipex Company, lililokuwa likiendeshwa na Maka Sebastian (26), ambaye amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa akiendelea na matibabu na basi aina ya Scania namba T438 CED mali ya kampuni ya Majinja lililokuwa likiendeshwa na Baraka Gabriel (38) aliyekufa papo hapo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi amesema chanzo cha ajali hiyo ni ubovu wa barabara katika eneo la ajali na mwendo kasi.
Baada ya magari hayo kugongana, kontena lililokuwa limepakiwa katika lori hilo lilifyatuka na kupiga basi hilo, hali iliyosababisha mauti kwa watu 50 na majeruhi wengi.

No comments: