Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
linamshikilia mkazi wa Mbagala Rangi Tatu, Haroub Mtopa (44) kwa kujifanya
mtumishi wa umma kupitia cheo cha Katibu wa Rais, Jakaya Kikwete, Prosper
Mbena.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema mtuhumiwa huyo
alikamatwa juzi jioni.
Kova alisema Mtopa alikuwa na mazoea ya kujifanya mtumishi wa Ikulu kwa
nia ya kudanganya watu kwamba anaweza kuwasaidia shida zao ili ajipatie fedha.
Katika kufanya kazi zake za kitapeli, Kova alisema mtuhumiwa huyo
alikuwa akiingia na kutoka Ikulu mara kwa mara, huku akijifanya kuwa na shida nyingi hivyo alikuwa akiomba
msaada.
‘’Huyu mtu ni tapeli wa muda mrefu sana, tulimkamata baada ya mwananchi
mmoja kuzungumza na mtuhumiwa huyo na kuahidiana kumpa Sh 500,000 na
kutanguliziwa Sh 250,000. Baadae aliitwa siku nyingine afuate fedha iliyobaki.
‘’Mwananchi huyo ambaye hakumtaja jina, alimhofia Mtopa ndipo alipotoa
taarifa Polisi kisha akamwambia
mtuhumiwa huyo aende kuchukua fedha iliyobaki, hatua iliyosaidia Polisi
kumkamata kwa urahisi,’’ alisema.
Kova alisema kuwa mtu huyo ni hatari kwa sababu kutumia cheo cha Katibu
wa Rais wakati inamaanisha kwamba mtu huyo aliweza kutapeli watu wengi sana
kupitia cheo hicho.
Kwa mujibu wa Kova, mtuhumiwa huyo amekuwa akizunguka katika wizara
mbalimbali ikiwamo ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Maji na taasisi nyingine zinazotoa huduma kwa
jamii, kwa lengo la kuomba msaada.
Alisema kabla ya kumkamata, walishirikiana na Ikulu baada ya watu wengi
kupeleka malalamiko yao kuhusu mtuhumiwa huyo.
Kova aliwaasa wananchi kuepuka kujifanya watumishi wa umma kwani ni kosa
kisheria na kuongeza kuwa wameweka kikosi maalumu kitakachoshughulikia masuala
ya watu wanaozunguka zunguka nje za ofisi za watu pasipo shughuli maalumu.
No comments:
Post a Comment