Katibu Mkuu wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amesema wizi ndani ya Serikali
ni moja ya mambo mawili yanayoangusha chama hicho na amewataka wanachama wake
kutoka kimya na badala yake, kupigia kelele vitendo vya wizi kwa watendaji wa
Serikali.
Katika hatua
nyingine, Katibu Mkuu huyo ameeleza kukerwa na dhana ya utawala bora, ambayo
amesema imekuwa ikitumiwa kama kivuli cha kulinda wezi wa mali ya umma, kwa
maelezo kuwa ni ngumu kuwafukuza madarakani au kuwaadabisha bila kufuata
sheria.
Alisema hayo
alipozungumza na wanaCCM wa Jimbo la Kibakwe mkoani Mpwapwa, akiwa katika ziara
ya kutembelea Mkoa wa Dodoma kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo, ikiwemo
utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010.
"Yapo
mambo yamewaudhi Watanzania wengi. Kwanza ni suala la wizi serikalini. Eti mtu
kaiba halafu sisi tunaanza kupiga maneno mara ooh kaiba au hajaiba? Aondoke
asiondoke?
“Tumwadhibu
tusimwadhibu? Ukweli ni kwamba mtu akituhumiwa, tuhuma peke yake inatosha
kumfanya aondoke na kama hataki basi tumuondoe kwa nguvu na si kuleta maneno,”
alisema na kuongeza kuwa enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, dhana
hiyo haikupewa nafasi kwa wezi.
"Lazima
niseme wazi, Watanzania wametushangaa sana katika hili, mwingine akiiba kuku si
sawa… wakubwa serikalini wanasema afungwe, lakini huyu aliyeiba fedha nyingi za
umma tunasema utawala bora!
“Lazima
tulikatae hili kwa nguvu zote na mtu wa kwanza
anayepaswa
kukasirika ni mwanaCCM, kuweni wakali acheni kabisa kulindana," alisema
Kinana.
Akionesha wazi
kukerwa na hali hiyo, Kinana alisema kinachosikitisha zaidi ni kuona mtendaji
ndani ya Serikali anapoiba, wanajitokeza wanaCCM wengine ili kumkingia kifua
asichukuliwe hatua, jambo ambalo limekuwa likiwakera Watanzania wengi.
"Mtu
ameiba wazi kabisa, wanatokea wanaCCM wenzake utasikia oooh hakujua, ooh
tumuonee huruma. Jamani huyu mtu hakujua kwani hana macho kuona anachokifanya
ni wizi?
“Nawaomba
wanaCCM simamieni uadilifu, mmechaguliwa na wananchi kutokana na imani yao
kwenu na kama tunavyofahamu imani huzaa imani, nataka niahidi CCM tutakuwa
wakali sana ukiiba lazima uondoke," alisema Kinana.
Akielezea
kukerwa na matumizi ya dhana ya utawala bora, Kinana alisema dhana hiyo katika
siku za hivi karibuni imeanza kutumiwa, ili kulinda wezi wa mali ya umma
wasichukuliwe hatua na kuadhibiwa kwa makosa wanayoyafanya.
"Siku hizi
kuna hiki kitu kimezuka kinaitwa utawala bora. Wakati mtu anaiba hafuati
utawala bora, lakini akishaiba na kukamatwa utasikia lazima tufuate utawala
bora, mara tuunde Tume, mara mpeni muda wa kujitetea, huyu mtu keshaiba
unapompa nafasi na tena kama ana fedha alizoiba anaweka mawakili hata wanne.
"Huu
utawala bora ni lazima sasa tuutazame kwa macho mawili maana ni kama umeegemea
upande mmoja. Mtu anaiba kuku hakuna utawala bora, lakini anaiba mali ya umma,
unaambiwa kuna utawala bora! Mwizi dawa yake ni jela si maneno, lazima tujenge
utamaduni wa kuwajibishana.
"Lazima
tuige wakati wa utawala wa Baba wa Taifa, yeye alisema ukikosea iwe ni sawa na
kugusa moto, ukigusa moto adhabu ni palepale, ilikuwa ukibainika tu
unastaafishwa kwa manufaa ya umma, lakini sasa unaambiwa utawala bora. Mtu
akiiba anahamishwa…
chama chenye
misingi imara siku zote kitaheshimika, kitaaminiwa na kitakaa madarakani kwa
muda mrefu.
"Mkilindana
wanaCCM na Iyena Iyena zenu hamtafika mbali, ni lazima sasa tuwe wakali. Wengi
wa wanaCCM ni masikini, na wachache kama 100 au 20 hivi ndio matajiri. Wanaiba, matajiri wachache wanaoishi maisha
ya mbinguni, adhabu wanapata masikini wengi wanaoishi duniani, hili
halikubaliki.
"WanaCCM
jumla yetu tupo milioni saba lakini hawa wezi wapo kama 100 au 20,
tusiyumbishwe na watu hawa wachache, mimi ni Katibu Mkuu wa Chama cha wakulima
masikini na
wafanyakazi masikini sitakubali kuona chama changu kinageuzwa dampo la
walanguzi," alisema Katibu Mkuu huyo wa CCM.
Kwa upande
mwingine aliwataka wanaCCM kutembea kifua mbele kutokana na utekelezaji mzuri
wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010, kutokana na mambo mengi yaliyoahidiwa katika
Ilani hiyo kutekelezwa japo alikiri kuwepo kwa changamoto kadhaa.
"Kama kuna
kasoro waite wananchi waambie, kama tunapongezwa kwa mazuri tuliyoyafanya ni
lazima tukubali kuulizwa maswali kwa yale ambayo hatujayatekeleza. Sio unataka
upongezwe kwa mazuri tu lakini mabaya tunayakwepa," alisema Kinana.
No comments:
Post a Comment