Jeshi la Polisi
mkoani Morogoro, linamshikilia mkazi wa Manispaa hiyo, Josephat Asenga (47),
mwenye taaluma ya uhasibu, kwa tuhuma za kujifanya Padri.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema kuwa, Asenga alikamatwa juzi
saa 10:30 jioni, katika maeneo ya Modeco, Kata ya Mazimbu katika Kanisa
Katoliki Parokia ya Mtakatifu Maria.
Kwa mujibu wa
Kamanda Paulo, mtuhumiwa huyo alifika parokiani hapo Juni mwaka jana akiwa
amevaa mavazi ya Padri na kujitambulisha kwa Paroko wa parokia hiyo, Malt
Dyfrig Joseph, kuwa yeye ni Padri anaishi Jimbo la New York Marekani.
Kwa mujibu wa
kamanda huyo, baada ya kujitambulisha kwa Paroko huyo na kuonesha kitambulisho
chake, alimuomba Paroko huyo kumpangia zamu ya kuendesha Misa ya Jumapili
iliyofuata na kukubaliwa na Paroko huyo bila kukagua vizuri kitambulisho chake.
Alisema mara
baada ya misa hiyo, Paroko alipata taarifa kutoka kwa msamaria mmoja wa Kituo
cha Amani cha Chamwino mjini hapa, kuwa Padri huyo feki anaishi na
mwanamke katika maeneo ya Ujenzi kinyume na taratibu za upadri.
Baada ya kupata
taarifa hizo, inadaiwa Paroko huyo aliwaomba waumini wamshawishi Padri huyo
feki, afike parokiani hapo na baada ya kufika, alihojiwa na Paroko huyo na
kudai kuwa alipata upadrisho katika Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa
kamanda huyo, baada ya Paroko huyo kupata maelezo hayo alifanya
mawasiliano na Katibu wa Jimbo hilo la Dar es Salaam na kujibiwa kuwa hakuna
jina la Padri huyo.
Juzi Alhamisi
majira ya saa 10:30, Padri huyo feki alimpigia simu Paroko huyo na kumuomba
ampange kuendesha Misa Takatifu ya Jumapili parokiani hapo, na kukubaliwa na
paroko huyo na kumtaka afike kanisani.
Baada ya
kufika, taratibu za kujulisha Polisi zilifanywa na askari walipofika kanisani
hapo, walimkamata mtuhumiwa huyo.
Kwa mujibu wa
Kamanda huyo, baada ya kufanya mahojiano na mtuhumiwa, alikiri kuwa yeye sio
Padri na walipokwenda nyumbani
kwake kwa ajili ya kufanya upekuzi, walimkuta akiwa na majoho saba ya upadri.
Mtuhumiwa huyo
ameendelea kushikiliwa Polisi na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi
kukamilika.
No comments:
Post a Comment