WAFANYAKAZI 300 WADHURIKA MGODINI BULYANHULU


Wafanyakazi zaidi ya 300 wa mgodi wa dhababu wa Bulyanhulu wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, wameachishwa kazi baada ya kupata madhara wakiwa kazini huku Bunge likieleza kwamba baadhi wako katika hali mbaya wakisaka msaada juu ya hatua hiyo.

Mgodi huo wa dhahabu wa Bulyanhulu, uko chini ya Kampuni ya African Barick Gold (ABG),  ambayo hivi karibuni ilibadili jina lake na sasa inatambulika kama Acacia Mining.
Mbunge wa Kisarawe, Suleiman Jafo (CCM) alisema jana bungeni kwamba wafanyakazi hao, wamekuwa wakihangaika katika ofisi mbalimbali, ikiwemo Wizara ya Kazi na Ajira kufuatilia suala hilo.
“Wamekuwa wakihangaika kutibiwa na wengine hali zao ni mbaya na mwenye kampuni anashindwa kuwahudumia,” alisema Jafo katika swali lake bungeni na kutaka kusikia kauli ya serikali juu ya watu hao na adha wanayoipata.
Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga,  alisema, suala hilo limechukua muda mrefu na limekuwa na utata mwingi.
Alisema suala hilo limekuwa likijadiliwa na linashughulikiwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA). “Na taarifa nilizo nazo, hata wiki iliyopita kulikuwa na kikao pale Osha  kujaribu kuona ni namna gani suala hili litafikia mwisho,” alisema Naibu Waziri.
Alisema, “lakini kwa kweli ni suala refu na Mheshimiwa Spika,  siwezi kuelezea kila kitu hapa. Lakini nimekuwa kwenye mchakato na makosa yamekuwapo kwa pande nyingi katika masuala haya yanayohusu wafanyakazi wa Bulyanhulu,” alisema Mahanga.
Swali hilo la nyongeza la Mbunge wa Kisarawe, lilitokana na swali la msingi la Mbunge wa Bukombe, Kulikoyela Kahigi aliyetaka kufahamu mpango ambao serikali inao wa kuwapatia pensheni kila mwezi wahadhiri wa vyuo vikuu, waliokuwa kwenye utaratibu wa mfuko wa zamani wa Senior Staff Superannuation Scheme (SSSS), waliostaafu kabla ya Machi 2011.
Vile vile Kahigi alitaka kufahamu serikali ina mpango gani wa kuwapatia pensheni wazee wote nchini, waliofikia umri wa kustaafu wa miaka 60.
Akijibu swali hilo, Mahanga alisema suala la wahadhiri wa vyuo vikuu waliokuwa kwenye utaratibu huo kabla ya kustaafu Machi 2011, bado linashughulikiwa na kwamba mazungumzo kati ya mwajiri (Chuo Kikuu) na Serikali bado yanaendelea.
Kuhusu pensheni kwa wazee wote, Mahanga alisema Serikali iko kwenye mchakato wa utafiti na majadiliano iweze kuanzisha programu ya Pensheni kwa Wazee wote.

No comments: