ELIMU HOLELA KATIBA MPYA MARUFUKU


Wakati nchi ikijiandaa kwa Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa, asasi za kiraia na kijamii nchini zinazotaka kutoa huduma ya elimu ya uraia na ya mpiga kura kuhusu Katiba Inayopendekezwa, zimetakiwa kuomba vibali vya kufanya hivyo, vinginevyo hazitaruhusiwa kutoa elimu yoyote juu ya katiba hiyo.

Agizo hilo lilitolewa jana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na ile ya Zanzibar (ZEC). Tume hizo zilisisitiza kuwa asasi zinapaswa kufanya hivyo kabla ya Februari 10 mwaka huu, yaani Jumanne ijayo.
Katika taarifa yake, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC,  Julius Mallaba alieleza kuwa kwa kuzingatia Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2013  Kifungu cha 5 na 6(1)(b), NEC na ZEC ndizo zilizopewa mamlaka ya kusimamia na kutoa kibali kwa Asasi za Kiraia na Kijamii ambazo zina nia ya kutoa Elimu ya Uraia na ya Mpiga Kura kuhusu Katiba Inayopendekezwa.
Aliongeza kuwa chini ya kifungu hicho cha sheria, Asasi ambayo haitapata kibali kutoka NEC na ZEC, haitaruhusiwa kutoa Elimu ya Uraia au Elimu ya Mpiga Kura kuhusu Katiba Inayopendekezwa.
“Pia Tume zinapenda kuzialika Asasi za Kiraia na Kijamii zenye nia ya kutoa Elimu ya Uraia au ya Mpiga Kura kuhusu Katiba Inayopendekezwa kuwasilisha maombi yao Makao Makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Posta House) na Makao Makuu ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Mtaa wa Maisara kabla ya tarehe ya mwisho ya kupokea maombi hayo Februari 10 mwaka huu,” alisema katika taarifa hiyo.
Pamoja na maombi hayo, asasi inayotaka kuwasilisha maombi yake inatakiwa ikidhi vigezo kama vile usajili kwa mujibu wa Sheria za Tanzania, iwe imefanya kazi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sio chini ya miezi sita toka isajiliwe kwake na iainishe majina ya viongozi wake.
“Vigezo vingine ni pamoja na kuwa tayari kujigharimia katika kutoa Elimu ya Uraia na Elimu ya Mpiga Kura, Isiwe na taarifa za kuvuruga amani au kuchochea fujo, watendaji wake wawe na uwezo wa kutosha wa kutoa Elimu ya Uraia na ya Mpiga Kura utakaoiwezesha Asasi hiyo kufanya kazi hiyo kwa ufanisi. Iwasilishe maeneo au majimbo inayotaka kutoa elimu hiyo, itoe na kukabidhi nakala za machapisho yatakayotumika na mwisho iwasilishe ratiba itakayoendesha elimu hiyo.
“Katika kutuma maombi hayo, asasi zote zinatakiwa kuambatanisha maombi yao na cheti cha usajili, katiba ya asasi, majina ya viongozi wa juu wa asasi, anuani kamili ya makazi na namba za simu za ofisini na za viongozi. Viambatanisho vingine ni zana za Elimu ya Uraia na Elimu ya Mpiga Kura (vijarida, vipeperushi, mabango, vipindi vilivyorekodiwa, fulana na kadhalika).
“Na mwisho kila asasi iambatanishe na ratiba itakayoonesha tarehe, mahali na muda watakaotoa Elimu ya Uraia na ya Mpiga Kura.”
Kwa mujibu wa sheria, Elimu ya Uraia na ya Mpiga Kura kwa ajili ya Katiba Inayopendekezwa, inapaswa kufanyika siku 60 kabla ya Kura ya Maoni.
Akizungumza mchakato huo juzi mjini Songea wakati wa maadhimisho ya Miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM, Rais Jakaya Kikwete alisema maandalizi ya Kura ya Maoni itakayopigwa Aprili 30 mwaka huu, yanaendelea kufanyika ili kuwezesha kura hiyo kutekelezwa kama ilivyopangwa.
Alitumia fursa hiyo kukitaka CCM kujipanga vizuri elimu kwa umma juu ya Katiba Inayopendekezwa na kampeni ya Kura ya Maoni.
Alisema: “Watani zetu watatoa elimu hasi kuhusu Katiba Inayopendekezwa, sisi tutoe elimu chanya. Wenzetu watataka Katiba Inayopendekezwa  isipite. Sisi tupige kampeni ikubalike. 
“Naomba msibabaishwe wala kudanganywa na watu wanaotaka kuturudisha nyuma kutoka katika hatua kubwa muhimu tutakazopiga kwa kuikubali Katiba Inayopendekezwa. Tusikubali kubaki nyuma,” alisema.

No comments: