Jaji
Mkuu, Mohamed Chande Othman amesema Kamati ya Maadili ya Majaji imeanza
kushughulikia tuhuma za kinidhamu na kimaadili dhidi ya majaji wawili wa
Mahakama Kuu, waliotajwa kupata mgawo katika fedha zilizochukuliwa kutoka
akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Majaji
hao, Aloysius Mujulizi anayedaiwa kupata Sh milioni 40.4 na Profesa Eudes
Ruhangisa pia anayedaiwa kupata Sh milioni 400.25 kutoka Mkurugenzi wa Kampuni
ya Kufua Umeme ya IPTL, James Rugemalila.
Jaji
Mkuu (pichani) alisema hayo katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi juzi kuhusu
hatua zinazochukuliwa na ofisi yake dhidi ya tuhuma za kinidhamu na kimaadili,
zinazowakabili majaji hao wawili.
Alisema
Kamati ya Maadili ya Majaji ilianza kazi yake Januari 26, 2015 na inaundwa na
jopo la majaji saba, ambapo wanne ni
kutoka Mahakama ya Rufaa na watatu wa Mahakama Kuu. Mwenyekiti wa Kamati hiyo ni Jaji
Mbarouk Salim Mbarouk. Wajumbe ni majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa ambao ni
Jaji Salum Massati, Jaji Katherine Oriyo na
Jaji Bethuel Mmilla. Wengine ni majaji watatu wa Mahakama Kuu,
ambao ni Jaji Augustine Mwarija, Jaji Aisha Nyerere na Jaji Imani Aboud.
Jaji
Mkuu aliwasihi wananchi kuvuta subira wakati suala hilo linashughulikiwa kwa
mujibu wa sheria na taratibu, zinahusiana na tuhuma hizo dhidi ya majaji hao.
Alifafanua
kwamba suala la kumwondoa kazini Jaji kwa tuhuma za kinidhamu au kimaadili au
mwenendo mbaya, lina awamu tatu ambapo kuanza kazi kwa tume hiyo ni awamu ya
kwanza.
Alisema
kamati hiyo itafanya kazi yake ya upelelezi na uchunguzi wa awali na kisha
ikiridhika kwamba tuhuma hizo zina uzito, basi itapeleka suala hilo kwenye Tume
ya Utumishi wa Mahakama na hatua ya mwisho katika suala kama hili ni kufikishwa
kwenye Tume ya Uchunguzi ya Kikatiba.
Alipoulizwa
juu ya shauku ya wananchi kutaka kufahamu muda unaoweza kutumika hadi kufikia
tamati ya suala hilo, Jaji Mkuu alisema:‘’ Kwenye kushughulikia suala hili
Kamati ya Maadili ya Majaji na Tume ya Utumishi wa Mahakama zitafanya kazi zake
kwa wakati.
‘’Lakini
haziwezi kuharakisha kwa kukiuka sheria na taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa
sheria. Kufanya hivyo kunaweza kubatilisha mwenendo mzima na hata maamuzi yao
iwapo yatapingwa mahakamani,’’ alifafanua Jaji Mkuu.
Aliongeza
‘’ni vyema tukangojea matokea ya kazi hii, ambayo inatakiwa ifanyike sio tu kwa
wakati, bali pia kwa weledi na umakini ili kila mmoja wetu aridhike kuwa haki
imetendeka na katiba, sheria na taratibu zimezingatiwa’’.
Kwa
upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Mark Bomani alipoulizwa
juu ya kuundwa kwa kamati hiyo ya Maadili ya Majaji, kuchunguza tuhuma hizo,
alisema hatua hiyo ni muhimu na haiwezi kupuuzwa pindi majaji wanapotuhumiwa.
‘’Tuhuma
kwa Jaji au Idara ya Mahakama ni lazima ichukuliwe kwa uzito mkubwa sana ili
tuhuma hiyo au hizo zisije zikaanza kuleta doa kwa usafi wa Mahakama kwani
Mahakama ni kioo cha jamii na kimbilio la wote wanaotaka haki”, alisema.
Alisema
ni vizuri wananchi wakaambiwa kwa uwazi juu ya hatua zinazochukuliwa kuhusu
suala hili ili kuwaondoa wasiwasi na kwamba linaweza kuchukua muda hadi kufikia
mwisho wake.
Alitoa
mfano kwamba yeye alikuwa mjumbe katika Tume ya Uchunguzi ya Kikatiba mwaka
1993, kushughulikia tuhuma dhidi ya aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu wakati huo,
John Mwakipesile dhidi ya tuhuma za mwenendo wake wa kikazi.
‘’Ilituchukua
mwaka mzima kukamilisha kazi hiyo na hatimaye kutoa mapendekezo yetu kwa Rais.
Wananchi wasilitazame hili kwamba litashughulikiwa haraka haraka na kumalizika
bali litachukua muda,’’ alisema.
Hatua
hiyo dhidi ya majaji hao ni utekelezaji wa Azimio la Tano, kati ya manane ya
Bunge kwa Serikali, juu ya sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, lililogubikwa na
ukiukwaji wa taratibu na sheria juu ya matumizi ya fedha hizo. Maazimio hayo
nane yalitolewa katika kikao kilichopita cha Bunge.
Azimio
hilo la Tano lilisema: “Bunge
linaazimia kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aunde Tume ya Kijaji
ya Uchunguzi kuchunguza utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na
Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania”.
Akihutubia Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam
Desemba 22, mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete alisema “Azimio hili nimelipokea,
tumelijadili. Hata hivyo, itabidi tufuate utaratibu wa kikatiba na kisheria wa
kushughulikia masuala ya namna hiyo. Inatakiwa suala kama hili lianzie kwenye
mhimili wa Mahakama yenyewe na siyo kwa Rais au Bunge. Tume ya Mahakama ndiyo
yenye mamlaka ya kumtaka Rais aunde Tume ya Kijaji ya kumchukulia hatua Jaji
yeyote pale inaporidhika kuwa amepoteza sifa za kuendelea kufanya kazi hiyo.
Nashauri suala hili tumuachie Jaji Mkuu wa Tanzania alishughulikie atakavyoona
inafaa”.
Akaunti
ya Tegeta Escrow ilifunguliwa BoT mwaka 2006 kwa ajili ya kuhifadhi fedha za
malipo ya tozo ya uwekezaji (capacity charges), zilizokuwa zinalipwa na Shirika
la Umeme nchini (TANESCO) kabla hazijakabidhiwa kwa anayelipwa, ambaye ni IPTL.
Kabla ya hapo, TANESCO ilikuwa inalipa moja kwa moja kwa IPTL.
Tayari
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka
ameondolewa katika nafasi hiyo kwa kuwekewa fedha katika akaunti yake Sh
bilioni 1.6 za mgao wa fedha za Tegeta Escrow. Waziri mwingine aliyejiuzulu kwa
sakata hilo ni wa Nishati na Madini, Profesa Sospetor Muhongo. Amejiuzulu kwa
madai ya kutoshughulikia ipasavyo suala hilo.
Kufuatia
sakata hilo, pia maofisa kadhaa wa BoT, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na
wengine kutoka Wizara ya Nishati na Madini, wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma
za fedha za akaunti hiyo ya Tegeta
Escrow.
Zaidi
ya Sh bilioni 300 zinasadikiwa kuchukuliwa kutoka katika akaunti ya Tegeta
Escrow kwa njia zisizo halali.
No comments:
Post a Comment