WABUNGE WAMKALIA KOONI WAZIRI NYALANDU AACHIE NGAZI


Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amebanwa bungeni huku baadhi ya wabunge wakimtaka ajiuzulu, kutokana na kile kilichoelezwa amesababisha Shirika la Hifadhi la Taifa  (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kupoteza Sh bilioni mbili kila mwezi.

Miongoni mwa wabunge waliosema Nyalandu anatakiwa kujiuzulu ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema). 
Wabunge hao walikuwa wakichangia taarifa ya utekelezaji wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.  
Zitto alisema Nyalandu ameikosesha serikali mapato kutokana na hukumu ya kesi, iliyofunguliwa na baadhi ya wamiliki wa hoteli katika hifadhi ya Taifa dhidi ya Tanapa, kupinga kuanza kutoza tozo mpya kwa mfumo wa Fixed Rate, badala ya mfumo wa zamani Concession Rate. 
Kwa mujibu wa Zitto, katika hukumu, Mahakama iliagiza wizara hiyo kutoa tangazo katika gazeti la serikali kuanza kutumika kwa tozo mpya.
Alisema takribani miezi minne sasa, tangu kutolewa kwa hukumu hiyo, Wizara haijatekeleza hukumu hiyo hali inayosababisha serikali kukosa mapato kwa kushindwa kukusanya kodi stahiki.
Zitto alishangaa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Mbunge wa Kahama, James Lembeli kushindwa kushughulikia suala hilo.
“Nimeshangaa katika hili, kama alivyosema Lema (Godbless-Mbunge wa Arusha Mjini) hivi karibuni kuwa kwenye wizara hii kuna mapacha watatu; yaani Mwenyekiti Lembeli, Waziri Kivuli wa wizara hiyo Mchungaji Peter Msigwa na Waziri Nyalandu wote mmeshindwa kulikemea hilo,” alisema. 
Aidha, alieleza kushangazwa na kile alichosema kamati hiyo kuishia kutaka serikali kufanyia kazi suala hilo huku nchi ikiendelea kukosa fedha. 
“Jioni ya leo nataka uwe umetoa tangazo serikalini kwa ajili hiyo lakini kama halijatoka Waziri awasilishe barua ya kujiuzulu kwa mwajiri wake kwa kukosesha serikali bilioni mbili (Shilingi) kila mwezi,” alisema.  
Awali Kamati kupitia kwa Mwenyekiti wake, Lembeli, ilieleza kuwa tangu kufunguliwa kwa kesi hiyo mwaka 2011 hadi Septemba mwaka jana, Tanapa imepoteza takribani Sh bilioni 80 kutokana na kukosa malipo ya tozo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kutoa hukumu ya kesi iliyokuwa imefunguliwa na baadhi ya wamiliki wa hoteli. 
Lembeli katika taarifa yake, alisema Kamati ilitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa imeishatoa tangazo katika gazeti la serikali ifikapo Januari 28 mwaka huu lakini haikufanya hivyo. Alitaka itoe maelezo juu ya sababu za kutotekeleza agizo hilo.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola alisema Waziri Nyalandu alimuahidi kushughulikia suala la wananchi kuliwa na mamba na viboko lakini hajatekeleza na kuhoji kama ameshindwa kuwadhibiti. 
“Wapiga kura wangu wanaliwa na mamba na viboko sasa nitapigiwa kura na nani kama wiki iliyopita kuna mwanamke ameliwa na mamba ambaye ni mpiga  kampeni wangu, sasa nani atanikampenia?” alilalamika.
Naye Mbunge wa Kwela, Ignas Malocha (CCM) alilalamika wapigakura wake kundelea kuliwa na mamba huku Waziri Nyalandu akimdanganya zaidi ya mara tatu.  
Alitaka Waziri kuacha kudanganya Bunge badala yake achukue hatua kwani wananchi wanateseka na kuuawa.  
Mbunge wa Ulanga Magharibi, Dk Hadji Mponda (CCM) alisema Waziri amepewa mamlaka na sheria ya wanyamapori kurudisha baadhi ya maeneo kwa wananchi lakini ameshindwa kufanya hivyo na kuacha wananchi wakiteseka.
Alisema yako mapori tengefu 42, lakini mengi hayana hadhi wakati wananchi wakiteseka kwa kuhofia kuyatumia huku Waziri akishindwa kutumia mamlaka aliyonayo.

No comments: