DEREVA WA OCD MANYONI AJIUA KWA RISASI

Askari aliyekuwa dereva wa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) Manyoni mkoani hapa, Aloyce Alibinus amejiua kwa kujipiga risasi mdomoni na kutokea kisogoni.

Kamanda wa  Polisi  Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka (pichani) alithibitisha tukio hilo huku akisema askari huyo alijiua jana  majira ya asubuhi  nyumbani kwake  kwa kutumia  bunduki ya jeshi hilo iliyokuwa na  risasi nane.
Alisema kabla ya kujiua, askari huyo aliyekuwa amejipumzisha nyumbani kutokana na kusumbuliwa na homa,  alitoka na kwenda kwenye  ghala  la silaha na kuomba apewe bunduki  moja kwa kile alichodai kuwa alikuwa na safari ya kikazi na bosi wake ambaye ni OCD.
Alieleza kuwa mtunza ghala hilo alimwamini na kumpatia bunduki  hiyo yenye risasi nane ambayo alikwenda  nayo  moja kwa moja nyumbani kwake na  kujifungia kisha kufungulia redio kwa sauti ya juu.
Aliongeza kuwa, askari huyo  alielekeza mtutu wa bunduki hiyo mdomoni  kwake na kujifyatulia risasi ambayo  ilipitiliza  hadi  kisogoni  hivyo kusababisha  kifo chake papo hapo.
Alisema  ingawa  uchunguzi  wa kina unaendelea kufanywa juu ya chanzo  cha askari  huyo  kuamua kukatisha uhai wake kwa kujiua, lakini  ujumbe  wa maandishi  aliouacha mezani umelitaka Jeshi la Polisi kutomsumbua mtu  yeyote, akisema amejiua kwa utashi wake.

No comments: