Wadau wa masuala ya kijamii nchini, wamepinga
kitendo cha kusimamishwa kazi kwa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya
Bandari Tanzania, Madeni Kipande.
Pia, wameomba Rais Jakaya Kikwete kuharakisha
uteuzi wa haraka Mkurugenzi wa TPA, badala ya kuiachia taasisi hiyo kuongozwa
na watu wanaokaimu nafasi ya ukurugenzi kwa muda mrefu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es
Salaam jana, Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii (CCK), Costantine Akitanda alisema
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta (pichani) alipaswa kuchukua muda zaidi,
kufahamu masuala mbalimbali yanayoendelea katika mamlaka hiyo.
Alisema kuwa Waziri alipaswa kutumia muda zaidi kujifunza kinachoendelea hivi sasa ndani ya TPA kupitia Bodi ya
Wakurugenzi ya mamlaka hiyo.
‘’Katika suala la zabuni tumeelezwa na watu walioko ndani ya TPA
kwamba Bodi hiyo kwa kushirikiana na menejimenti chini ya Kipande, wamekuwa wakali kuepusha uwezekano wa watu wasio na
sifa stahiki kushinda zabuni zinazotangazwa na Mamlaka ya Bandari,’’
alisema Akitanda.
Pia, alisema kwamba kwa muda mrefu wajanja
wengi walikuwa wanajipenyeza kwenye zabuni na kufanikiwa kufanya kazi na
TPA kutokana na udhaifu uliokuwepo kwenye usimamizi wa sheria.
Aliongeza kuwa ukali uliooneshwa na Kipande kwa kushirikiana na Bodi hiyo, ndio uliofanya watu wasioitakia
mema TPA, wajipenyeze haraka kwa Waziri Sitta na kumpotosha kuhusu utendaji wake.
“Sitta alipaswa kushirikiana na bodi ili
kupata maelezo ya kutosha kuhusu utendaji wa Kipande na pia
angemueleza tuhuma hizo na kumpa fursa za kujieleza badala ya kufanya
maamuzi ambayo tunaweza kusema ni yasiyo sahihi,’’ alisema Akitanda.
Alisema katika kipindi alichofanya kazi
Kipande, masuala ya wizi yamepungua TPA na kwamba mapato ya nchi yameongezeka hali
ambayo inaleta aibu kwa kumsimamisha kazi.
Alifafanua kuwa aliyekuwa Waziri wa Wizara
hiyo, Dk Harrison Mwakyembe wakati akisimamia mamlaka hiyo, bandari ilikuwa
inahudumia tani milioni 14 kutoka tani milioni 12.5 mwaka juzi.
Pia, alisema wafanyabiashara wa ndani na nje,
wamesikitishwa na hatua hiyo kutokana na kusimamishwa mara kwa mara kwa
viongozi wa bandari.
No comments:
Post a Comment