WIZARA YA NISHATI YAMTISHA WAZIRI, ATAKA AOMBEWE


Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene ameomba aombewe afanye vizuri asipeleke aibu nyumbani, kwa kile alichoeleza wizara anayoongoza ni ngumu.

Alisema ugumu wake unatokana na wizara hiyo kubeba rasilimali za nchi.
“Niombeeni kwa Mungu, wizara hii inahusika na rasilimali za nchi, ni wizara nzito, kazi ni kubwa tunalinda mafuta, madini, gesi na umeme, sioni sababu ya kujisifu wala kustahili  kuliko wengine. Mnisaidie kwenye maombi ili nifanye vizuri nisilete aibu nyumbani,” alisema.
Simbachawene ambaye ni Mbunge wa Kibakwe mkoani Dodoma,  alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na wananchi wa Mpwapwa na wapiga kura wake, waliojitokeza kumlaki na kumpongeza kwa  kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Alisema  kuteuliwa kushika wadhifa huo ni jambo moja  na anahitaji maombi aweze kutekeleza wajibu, kutokana na wizara hiyo kubadilishwa mawaziri na manaibu waziri kila mara.
Alisema kwenye wizara hiyo kuna watu wanaotaka vitalu, kuna watu wanaopora maeneo na wanaotaka kupora mali za Watanzania, licha ya wao pia kuwa watanzania.
“Pamoja na kulinda mali za Watanzania nina wajibu wa kuhakikisha nishati inapatikana kwa watu wote na sasa serikali iko katika mpango kamambe wa kusambaza umeme vijijini,” alisema.
Alisema dhamira ya serikali ni kuhakikisha vijiji vyote vinakuwa na umeme kwa lengo la kuwafanya Watanzania kuwa na maisha bora.
Licha ya kukabidhiwa zawadi mbalimbali wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Kibakwe,  pia wazee walimkabidhi  Sh 100,000 kwa ajili ya kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea tena ubunge jimboni humo.
Aidha, viongozi wa dini walimfanyia maombi. “Nashukuru kwa mapokezi makubwa na ukarimu mkubwa mliouonesha  na nawaahidi sitawaangusha,” alisema.
Awali, kabla ya kufika Kibakwe, waziri huyo alisimamishwa mara kwa mara njiani na wananchi waliokuwa wamebeba mabango.
Katika vijiji vya Lukole na Kilolo, wananchi walisema wanahitaji umeme kwani maisha yao yamekuwa magumu kutokana na kutembea umbali mrefu kutafuta mashine za kusaga.
“…Tunaomba utusaidie tupate umeme. Sisi akina mama tunatembea umbali mrefu kwenda kusaga tunaporudi tumechelewa ugomvi moja kwa moja ndani ya nyumba,” alisikika mama mmoja akilalamika.
Waziri alimtaka Meneja wa Shirika la Umeme (Tanesco) Mkoa wa Dodoma, Zakayo Temu kuhakikisha kijiji hicho kinapatiwa transfoma umeme uanze kusambazwa.
“Nimeshatoa maagizo na meneja kanihakikishia hadi Juni mwaka huu, zoezi hilo litakuwa limekamilika,” alisema na kuwataka wananchi kufanya haraka kufunga nyaya za umeme na taa kwenye nyumba zao.
Pia, wananchi wa Kijiji cha Kingiti waliziba njia kwa mabango kuomba kupatiwa zahanati. Aidha, katika Kijiji cha Idunda wananchi hao waliomba kupatiwa umeme kutokana na kuchoka kutumia koroboi.
Wananchi hao waliahidiwa kupatiwa umeme haraka iwezekanavyo. Aliahidi kutoa mabati kwa ajili ya kuezeka zahanati ya Kingiti.
“Upatikanaji wa umeme vijijini utaimarisha uchumi, kwani wananchi watakuwa na uwezo wa kuanzisha viwanda vya usindikaji,” alisema.
Alisema licha ya serikali kutumia fedha nyingi kusambaza umeme vijijini, changamoto kubwa iliyopo ni wananchi kushindwa kuunganisha umeme unapofika kwenye maeneo yao.
 “Tumieni nishati kuboresha maisha yenu, jipangeni ili muweke umeme, umeme umefika kwenye vijiji vingi lakini watu bado hawaunganishi kwenye nyumba zao wakati walitakiwa kutumia fursa hiyo hata kuwa na viwanda vidogo vya usindikaji,” alisema.

No comments: