WABUNGE WATAKA JWTZ WAPEWE JUKUMU LA KULINDA RAIA


Serikali imehadharishwa juu ya uvamizi na wizi wa silaha katika vituo vya polisi, kwa kuambiwa hali hiyo inatisha na kuhitaji hatua za makusudi kuimarisha ulinzi nchini.  

Baadhi ya wabunge wameshauri Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), yaruhusiwe kusaidia Polisi kulinda raia na mali zao, hususan kudhibiti vikundi vya kihalifu vinavyojitokeza.  
Akichangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama iliyowasilishwa bungeni, Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM) alisema vituo vya polisi kuvamiwa na majambazi na kuibiwa silaha, ni hali inayotisha ikidhihirisha uhalifu ulivyokithiri nchini.
“Tuyaombe majeshi mengine ya ulinzi ya nchi yasaidie jeshi la polisi. Kama tuliweza kutumia majeshi mwaka jana kupambana na majangili, leo tunashindwa nini kupambana na wahalifu hawa waliokithiri?
“Si dhambi kutumia askari wa JWTZ au JKT kulinda nchi yetu. Eti wanajeshi wetu wako nje ya nchi wanalinda wananchi, lakini ndani ya nchi yetu wananchi wanaumia.”
Alisema magenge ya kihalifu, wizi na uhalifu unaojitokeza unatisha sana. Alitoa mfano wa kuibuka kwa kikundi cha Panya Road jijini Dar es Salaam na kusema askari ama kwa uchache au kwa kukosa vitendea kazi, wanashindwa kudhibiti uhalifu.
Alitoa mifano mingine ya uhalifu ni pamoja kukithiri kwa wizi wa kutumia pikipiki na kusema imefikia hatua, watu wanaoporwa wameviona vitendo vya kawaida kwa kutokwenda kuripoti polisi.  
“Kama hatuwezi kuajiri askari wa kutosha kwenye jeshi la polisi tukawapa vitendea kazi jeshi la polisi, wakapewa makazi bora, ulinzi au usalama utakuwa katika hali ya hatari huko tuendako,” alisema.  
Akihimiza majeshi kutumika kudhibiti makundi ya kihalifu yanayojitokeza kwenye jamii, mbunge huyo alisema, "Majeshi, hasa JKT wako vijana wengi kambini. Kwa nini tusiwatumie? Tunaona shida gani kuwatumia? Si suala la kukaa na kusema, kimataifa jeshi hawaruhusiwi kulinda.” 
Awali, Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, katika taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake kati ya Februari mwaka jana na Januari mwaka huu, ilisema ilibaini katika kipindi hicho hali ya ulinzi wa nchi na usalama wa raia ilikuwa shwari.
Kamati kupitia kwa Mjumbe wake, John Chiligati ilipongeza jeshi la polisi kwa jitihada  za kudhibiti uhalifu nchini.
“Kamati ilipotembelea Mkoa wa Arusha iliridhika na hali ya kupungua matukio ya uhalifu na pia ilikuta hali ya utulivu na amani imerejea katika Jiji la Arusha,” alisema Chiligati.  
Hata hivyo, kamati ilishauri polisi itafute njia mbadala na za kisasa za kupambana na kudhibiti uingizaji nchini wa dawa za kulevya, ukiwemo usafirishaji bangi kwenda Kenya na uingizaji mirungi nchini kutoka kutoka nchi hiyo.  
Aidha, ilishauri polisi kwa kushirikiana na jamii iongeze jitihada na ibuni mbinu mpya za kudhibiti wale wote wanaoendesha uhalifu na uuaji wa watu wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe.  

No comments: