MTUHUMIWA AUA POLISI KWA PANGA DODOMA


Polisi mkoani Dodoma wanamsaka mkazi wa Chang’ombe Juu, Tisi Malya kwa kumuua askari polisi kwa kumcharanga mapanga wakati akijaribu kumuokoa mtoto wa miezi minane aliyekuwa anataka kuuawa na mtu huyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime amemtaja askari aliyeuawa majira ya saa 5:00 asubuhi kuwa ni Joseph Swai.
Akisimulia mkasa huo kwa waandishi wa habari, Kamanda Misime alisema kuwa askari huyo aliitikia mwito uliofika kwake wa kuwepo kwa dalili ya tendo la jinai nyumbani kwa mkazi mmoja wa Chang’ombe Juu katika Manispaa ya Dodoma.
Alisema askari huyo alipigiwa simu na Mtendaji wa Mtaa wa Chang'ombe Juu, akimjulisha kuwa amepokea taarifa ofisini kwake kutoka kwa Oliver Baltazar
(52) mkazi wa Chang'ombe Juu kuwa mtoto wake, Tisi Sirili anaonekana anataka kumuua au ameshamuua mtoto wake wa miezi minane, Valerian Tisi.
Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo, askari huyo alikwenda ofisini kwa mtendaji huyo ambapo waliongozana hadi nyumbani kwa mtuhumiwa.
"Alipofika askari aligonga mlango huku akijitambulisha kuwa yeye ni askari ili mtuhumiwa atoke nje, alichofanya mtuhumiwa ni kumnyanyua mtoto wake mdogo wa miezi minane kwa mkono mmoja kichwa chini miguu juu na kutaka kumkata kwa panga huku akisema, ‘namkata shingo na sitaki kuona mtu’.
"Askari aliamua kumwokoa mtoto huyo kwa kumrukia mtuhumiwa, lakini kwa bahati mbaya aliteleza na ndipo mtuhumiwa akamkata kichwani askari wetu," alisema Misime.
Alisema pamoja na askari huyo kuanguka, mtuhumiwa aliendelea kumkatakata kwa panga huku mtendaji na kijana waliyekwenda naye eneo la tukio, wakikimbia huku wakipiga kelele za kuomba msaada.
Alisema mtuhumiwa baada ya kufanya kitendo hicho cha kinyama, alikimbia akiwa na panga lake huku nguo zake zikiwa zimetapakaa damu.
Aidha, alisema katika hekaheka hizo, mama wa mtoto baada ya kuona mtoto amebwagwa na askari ameanguka  chini, naye alimkwapua mtoto na kukimbia naye mahali pasipojulikana. Alisema polisi wanamsaka  baba huyo na mama huyo  kwa ajili ya usalama wake.
*Picha iliyotumika imetoka Maktaba.

No comments: