UANDIKISHAJI KIELEKTRONIKI KUHADILIWA NA BUNGE, SERIKALI


Bunge limeingilia kati mchakato wa uandikishaji wapigakura kwa mfumo wa kielektroniki (BVR) chini ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa kuamua  kujadili kile kilichoelezwa kwamba tume imekiuka makubaliano kwa kuanza mchakato bila  kushirikisha vyama vya siasa.  

Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu (pichani) aliagiza Serikali, Kamati ya Uongozi ya Bunge na Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia, wakutane kujadili suala hilo baada ya mbunge huyo kulifikisha bungeni kupitia mwongozo wa Spika, akilalamika wadau kutoshirikishwa.
“Jana (juzi) Tume ya Taifa ya Uchaguzi, imeanza kufanya utaratibu wa zoezi katika Mkoa wa Lindi, Mkoa wa Mtwara, Mkoa wa Rukwa, na Mkoa wa Njombe bila wadau wakuu kushirikishwa kama tulivyokubaliana,” alisema Mbatia.
Kwa mujibu wa Mbatia, katika kikao cha Januari 8 mwaka huu, cha wadau ambao ni vyama vya siasa vinavyounda TCD, NEC iliwahakikishia kwamba kabla ya mchakato kuanza Februari 15 mwaka huu, ingekaa nao kujadiliana na kufikia makubaliano.
Baada ya Mbatia kuomba mwongozo wa kiti, Zungu alisema; “Nakubaliana na wewe ni jambo muhimu, nakubaliana na wewe tukae pamoja, nakubaliana na wewe Bunge ni chombo kikuu cha kusimamia serikali.”
Zungu alisema, “Nakubaliana tukae pamoja, naagiza Waziri wa Fedha, Serikali na Mbatia tukae kama  Kamati ya Uongozi,” alisema Zungu na kukabidhi jukumu la kuendesha kikao kwa Mwenyekiti mpya, Lediana Mng’ong'o aliyechaguliwa juzi. 
Awali, baada ya kipindi cha maswali na majibu, Mbatia aliomba mwongozo kwa kuzingatia Kanuni ya 47 inayoruhusu  mbunge kuomba jambo halisi la dharura lenye maslahi kwa taifa, kuwasilishwa bungeni na kujadiliwa na wabunge. 
Alisema jambo hilo lenye maslahi kwa umma ni kuhusu BVR. Alisema nchi haina daftari la wapigakura na kwamba Julai 9 mwaka jana, NEC ilipokutana na wadau iliwaambia daftari lililopo halifai na kwamba wameanzisha utaratibu wa kuanzisha jipya kwa wapiga kura wote. 
Alisema walitaarifiwa kwamba mfumo utakaotumika ni mpya wa kielektroniki.  Alisema tume iliahidi kwamba mwanzoni mwa Septemba uandikishaji ungeanza, lakini haikuwa hivyo.
Baadaye walisema mwishoni mwa mwezi huo, pia haukufanyika. Hata hivyo, alisema Desemba mwaka jana, walifanya majaribio ya uandikishaji  katika majimbo yaliyopo mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Katavi.
Kwa mujibu wa Mbatia, Januari 8 mwaka huu, wakiwa na kikao cha wadau wa vyama vya siasa vinavyounda TCD, Mwenyekiti wao, wakati huo John Cheyo alifanya juhudi kualika NEC kuhudhuria. 
Alisema kwenye kikao hicho, Tume iliwahakikishia kuwapo changamoto nyingi zinazokabili mchakato huo wa uandikishaji.
Mbatia alisema waliambiwa mchakato utaanza Februari 15. Mbunge huyo alisema tume iliwaahidi kwamba, baada ya Februari 12, NEC itakaa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kujadili kwa pamoja kabla ya kurudi kwa wadau (vyama) kuwaelimisha namna mchakato huo wa uandikishaji utakavyofanyika, ikiwemo matumizi ya mfumo huo wa kielektroniki kisha wakubaliane.
Hata hivyo, alisema wameanza kwenye mikoa kadhaa bila kuwahusisha.  Alisisitiza kwamba,  wadau hao ambao wote ni vyama vya siasa chini ya viongozi wake wakuu, katika kikao hicho, walishauri NEC wakae pamoja kuziba nyufa, waaminiane na mchakato ufanyike kwa uaminifu wa hali ya juu kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani. 

No comments: