Kiongozi wa Kanisa la Waadventista
Wasabato (SDA) duniani, Askofu Ted Wilson anatarajiwa kuwasili nchini leo kwa
ziara ya kikanisa ya siku nne.
Taarifa iliyotolewa na kanisa hilo,
jijini Dar es Salaam, inaonesha kuwa
kiongozi huyo anakuja nchini kushiriki Sherehe za Utume zilizoandaliwa na
kanisa hilo na kujumuisha nchi zingine 11 za Afrika Mashariki na Kati.
Pamoja na kushiriki kwenye sherehe hizo,
lakini kiongozi huyo atashiriki kwenye kuzindua miradi mbalimbali ya afya na
elimu ya kanisa hilo nchini.
Sherehe hizo ambazo zinatarajiwa kuvuta
zaidi ya watu 50,000 kutoka nchi hizo 11 na sehemu zingine duniani, zitakwenda
sambamba na utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii, ikiwa ni pamoja kupima afya
kwa magonjwa mbalimbali kama ya moyo, sukari, Ukimwi na magonjwa mengine.
Juzi Kiongozi wa Mawasiliano wa kanisa
hilo katika ukanda wa Kati na Mashariki mwa Afrika, Mchungaji Steven Bina
alisema mkutano huo wa siku nne, ambao unafanyika Uwanja wa Taifa ni wa aina
yake na wa kwanza kufanyika nchini.
Katika mfululizo wa sherehe hizo, jana
kulizinduliwa ujenzi wa Makao Makuu ya Jimbo la Kusini Mashariki mwa Tanzania
(SEC), ambayo yatajengwa katika maeneo ya Kwembe, nje kidogo ya Dar es Salaam.
Shughuli zingine ambazo zilifanyika
juzi ni uzinduzi wa kituo cha vitabu, ambacho kipo eneo la Ilala na kitatoa
huduma kwa wakazi wa Dar es Salaam, ambao watahitaji vitabu mbalimbali vikiwemo
vya afya na aina vya vyakula vinavyofaa kwa mwili wa binadamu. Kituo hicho
kilizinduliwa na Mkurugenzi wa Idara ya Uchapishaji ya kanisa hilo duniani,
Mchungaji Howard Faigao.
Miongoni mwa shughuli zingine ambazo
zitafanywa na kanisa leo ni utoaji wa vitabu 1,000 na jozi 300 za viatu kwa
ajili ya shule za msingi, na utoaji wa vifaa vya maabara kwa ajili ya shule za
sekondari. Vitu hivyo vitatolewa kwa manispaa ya Ilala, ambayo ndio
itakayovisambaza mahali ambako kuna mahitaji.
Mkutano huo unahusisha washiriki kutoka
nchi za Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC), Eritrea, Somali, Ethiopia, Sudan Kusini na Djibout. Baadhi ya
kwaya pia zitatoka nje ya Bara la Afrika.
Tamasha hilo kubwa la kitume,
linatarajiwa kuhutubiwa kesho na Rais Jakaya Kikwete. Lakini pia kutakuwepo na
viongozi wengine wapatao 400 wa kanisa hilo kutoka ukanda wa Afrika Mashariki
na Kati.
Sherehe hizo zenye kauli mbiu ya
“Kusherehekea Mibaraka ya Mungu katika
Utume”, zinafanywa na kanisa hilo ikiwa ni njia ya kujivunia mafanikio makubwa
yaliyofikiwa katika upelekaji wa injili na utoaji wa huduma za jamii.
No comments:
Post a Comment