YANGA YAITUNGUA AZAM KILELENI LIGI KUU YA VODACOM

Timu ya soka ya Yanga imefanikiwa kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu baada ya kuifunga Coastal Union bao 1-0 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Yanga ambayo Jumapili iliyopita ililazimishwa sare ya bila kufungana na Ndanda FC, kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam pamoja na ushindi huo, ilionyesha kiwango kibovu kwa kuiga mpira uliokuwa unachezwa na wenyeji wao Coastal Union.
Bao pekee la Yanga katika mchezo huo lilifungwa katika kipindi cha kwanza na nahodha wake Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwa kichwa, akiunganisha mpira uliokuwa umerushwa na Mbuyu Twite dakika  ya 11 ya mchezo huo ulioshuhudiwa na mashabiki wengi wa Jijini Tanga na mikoa jirani.
Kiungo Abdulhalim Humud  wa Coastal Union alikaribia kuisawazishia timu yake bao dakika ya 39, baada ya kupiga mpira wa adhabu ndogo nje ya kisanduku cha penalti, lakini mpira wake ulipanguliwa na kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’ na kumkuta Ramadhan Salim aliyeshindwa kuukwamisha wavuni na kuokolewa na walinzi wa vijana hao wa Jangwani.
Hadi mwamuzi Athuman Lazi wa Morogoro anapuliza kipyenga cha mapumziko, Yanga ilikuwa mbele kwa bao hilo la Cannavaro lakini ilikuwa imezidiwa na Coastal Union ambao walifanya mashambulizi mengi zaidi kwenye lango lao na kupoteza nafasi nyingi kupitia kwa washambuliaji wake, Salimu na Hussein Sued.
Wenyeji Coastal Union walikianza kipindi cha pili kwa kasi wakiwa na lengo la kusawazisha bao hilo na kufanya mashambulizi kwenye lango la Yanga na katika dakika ya 49 Itubu Imbemu alikosa bao la wazi baada ya kupiga shuti kali akiwa ndani ya eneo la hatari, lakini Barthez alilipangua na Rajabu Zahiri kuondosha mpira huo kwenye hatari.
Coastal Union inayofundishwa na kocha James Nandwa raia wa Kenya, ilijitahidi kupanga mashambulizi yake na kulishambulia mfululizo lango la Yanga, lakini washambuliaji wake Sued na Mnigeria Imbemu walishindwa kuzitumia vizuri nafasi za kufunga walizozipata.
Yanga ambao walionekana kucheza kwa kujihami zaidi huku wakitumia mipira mirefu dakika ya 55 nusura ipate bao la pili kupitia kwa Amisi Tambwe aliyekuwa akijiandaa kuunganisha pasi ya Kpah Sherman lakini beki wa Coastal Union, Tumba Sued aliutoa mpira huo nje na kuwa kona.
Beki wa Coastal Union, Tumba alijikuta akioneshwa kadi ya njano dakika ya 58 kwa kumchezea vibaya Sherman wa Yanga na dakika moja baadaye kocha  Nandwa alifanya mabadiliko kwa kumtoa Imbemu na nafasi yake kuchukuliwa na Keneth Masumbuko dakika ya 59. 
Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm naye alikifanyia mabadiliko kikosi chake kwa kumtoa kiungo Mbrazili Andrew Coutinho na Tambwe ambao nafasi zao zilichukuliwa na Hussein  Javu na Danny, lakini mabadiliko hayo hayakubadili matokeo ya mchezo huo.
Zikiwa zimesalia dakika mchezo huo kumalizika, Sued wa Coastal Union alikosa bao la wazi akiwa na kipa Barthez baada ya kutengenezewa pasi safi na Masumbuko, lakini shuti alilopiga halikulenga lango.
Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 22 na kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara baada ya kucheza mechi 12 huku ikiipiku Azam iliyopo nafasi ya pili, ikiwa na pointi 21 na mchezo mmoja kibindoni.

No comments: