TAKUKURU YASEMA IKO TAYARI KWA UCHAGUZI MKUU



Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) imesema imejipanga kikamilifu kuhakikisha inashughulikia vitendo vya utoaji na upokeaji rushwa katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Akizungumza jana wakati wa ufunguzi wa jengo la taasisi hiyo mkoani Kigoma lililogharimu Sh bilioni 1.2, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hosea alisema anasubiri kuanza kwa ratiba ya Tume ya Uchaguzi ili iweze kuanza kutekeleza jambo hilo kwa kufuata sheria za uchaguzi.
Alisema taasisi yake imeshaanza kuona viashiria vya utoaji rushwa vinavyofanywa na baadhi ya watu walioonesha nia ya kugombea katika uchaguzi mkuu ujao kwa kutoa vitu mbalimbali zikiwemo fulana, chupa za chai na vitu vinavyofanana na hivyo.
Hata hivyo, alisema kwa sasa haitaweza kuwakamata wala kuwahoji watu hao kwa kuwa si wagombea rasmi kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi, lakini alibainisha kuwa vijana wake wanafuatilia kwa karibu nyendo zinazofanywa na watu hao.
Sambamba na kujipanga, Hosea alitoa wito kwa wananchi kuchukia vitendo vya kupokea rushwa wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu kwani vinawapotezea haki ya kuchagua mgombea mwenye sifa badala yake hushawishiwa kuchagua kwa rushwa.
Katika hatua nyingine, Dk Hosea alisema serikali imeokoa kiasi cha Sh bilioni 39 ambazo zilikuwa zilipwe kwa watu mbalimbali ambao hawakufuata sheria na taratibu za malipo na manunuzi.
Awali, Katibu Tawala wa mkoa Kigoma, Dk John Ndunguru alisema kuboreshwa kwa mazingira ya kufanyia kazi katika maeneo yenye mazingira magumu kunatoa unafuu kwa watu wanaopangwa maeneo hayo kuripoti na kufanya kazi.
Akizungumzia uchaguzi mkuu ujao, Ndunguru aliitaka Takukuru kutoa elimu kwa jamii kujiandikisha na kupiga kura kwa wagombea watakaosimamia maendeleo yao, badala ya kuchagua wagombea wanaotoa rushwa.
Naye Mkuu wa Takukuru mkoani Kigoma, Susan Lyimo alisema pamoja na mafanikio mbalimbali, ofisi ya taasisi hiyo mkoani Kigoma inakabiliwa na changamoto ya   mashahidi kushindwa kujitokeza kutoa ushahidi katika kesi za rushwa.
Alisema jumla ya kesi tisa za watu wanatuhumiwa vitendo mbalimbali vya utoaji na upokeaji wa rushwa zipo mahakamani zikiwa katika hatua mbalimbali.

No comments: