MAMIA WAJITOKEZA MAZISHI YA FAMILIA ILIYOTEKETEA MOTOMakamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal jana aliwaongoza mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, kuzika miili ya watu sita wa familia moja waliokufa katika ajali ya moto wakiwa nyumbani kwao Kipunguni, Manispaa ya Ilala usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita.

Katika maziko hayo yaliyofanyika makaburi ya Airwing yaliyopo Ukonga Banana, ibada ya maziko iliongozwa na Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigirwa akisaidiwa na mapadri watano.
Umati wa wananchi ulianza kufurika mapema, ingawa shughuli ya kuihifadhi miili ya marehemu hao ilianza saa 7:08, baada ya kuwasili kwa Makamu wa Rais na kuendelea kwa saa sita mfululizo hadi takribani saa moja usiku.
Makaburini hapo, majeneza sita yalipangwa kila moja karibu na kaburi, huku baba wa familia, David Mpira akitangulia kuzikwa kwa kutanguliza kiungo cha mguu wake kilichotambuliwa jana asubuhi chumbani kwake na baadaye kuwekwa jeneza na kuzikwa rasmi.
Mpira, aliyekuwa askari mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), hadi mauti yanamfika alikuwa Katibu wa kikundi cha wanamaombi wa kanisa hilo.
Baadaye alizikwa mke wa Mpira, Celina Yegela (50) aliyekuwa mstaafu wa Shirika la Usafirishaji Mizigo kwa Njia ya Ndege (DAHACO). Wengine waliokufa katika ajali hiyo na kuzikwa jana ni Samuel Yegela aliyekuwa anajiuguza nyumbani kwa dada yake, Lucas Mpira mtoto wa familia hiyo na wajukuu wake, Celina na Paulina Emmanuel.
Ndugu wa marehemu, wakiongozwa na mtoto pekee wa familia hiyo aliyenusurika, Emmanuel Mpira, baba wa watoto wawili waliokufa ambaye amepoteza pia wazazi wawili, mjomba na kaka yake, waliangua vilio vya mara kwa mara huku baadhi yao wakipoteza fahamu.
Awali, mara baada ya kuwasili kwa miili yao, Makamu wa Rais aliongoza kutoa heshima kwa marehemu hao kwa kuangalia picha zao, akifuatiwa na Askofu Nzigirwa, Mawaziri Profesa Mark Mwandosya na Dk Harrison Mwakyembe, Naibu Waziri Dk Milton Makongoro Mahanga, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki, wanafamilia na baadaye waumini wachache waliowakilisha umati wa wananchi waliohudhuria.
Katika ibada hiyo, Askofu Nzigirwa alitoa salamu kutoka Jimbo Kuu la Dar es Salaam na kusema msiba huo ulikuwa mzito, kutokana na kuondoa familia yote kwa wakati mmoja, huku akisema majibu ya maswali waliyonayo watu wengi yapo kwa Mungu.
“Tumesikia kuwa vifo hivi vimetokana na ajali, hivyo tunajiuliza kwa nini wasingeacha kuangalia televisheni wasingekufa au vikosi vya ukoaji wangewahi wasingekufa, ni vyema kuacha kujiuliza kwa nini, bali tumuombe Yesu awapokee katika ufalme wake,” alisema.
Alisisitiza kuwa, familia hiyo ilikuwa ikiishi kwa kumtumainia Mungu na kwamba hata kama walikuwa na mapungufu yao, lakini hawakumwacha Mungu, hivyo tukio hilo la kuchukua familia na watu wa rika tofauti, linafundisha jamii kuishi kwa kumtumikia Mungu.

Makamu wa Rais, akizungumza katika maziko hayo, alisema msiba huo ni mkubwa na aliwapa pole wafiwa na kuwaomba kuwa na moyo wa subira huku akiwaombea marehemu miili yao ilale mahali pema peponi.
Aliwasihi Watanzania kujitahidi katika nyumba zao kuwa na vizimia moto na kuhakikisha wanajitahidi  kuweka madirisha au milango  ya dharura kwenye nyumba zao.
Aliwataka wakati wa matukio ya moto, kuhakikisha wanapiga namba ya zimamoto 114 badala ya kupiga namba za polisi.

No comments: