TAKUKURU YAAPA KUTOACHA MTU SAKATA LA ESCROW


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema kuwa haikurupuki katika kuwashughulikia na kuwafikisha mahakamani viongozi wanaotuhumiwa kujipatia fedha kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow na kwamba ushahidi pekee ndiyo itakaofanya kuwafikisha mahakamani watuhumiwa.

Akizungumza mara baada ya kuzindua jengo la ofisi ya mkoa la Taasisi hiyo mjini Kigoma juzi, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alisema hakuna atakayeachwa katika sakata hilo iwapo ushahidi utathibitisha pasi na shaka kwamba alihusika.
Alisema uchunguzi dhidi ya viongozi na watu mbalimbali waliohusina na uchotaji wa fedha hizo unaendelea na kwamba ushahidi utakapokamilika kila mmoja atapata kile anachostahili bila kumuonea mtu.
“Hatutaki kukurupuka katika kushughulikia watuhumiwa wa sakata la Escrow na muhimu ni ushahidi ambao utawatia hatiani watuhumiwa, ni aibu kwangu kumfikisha mtuhumiwa mahakamani na mwisho wake siku ushahidi hautoshi na mtuhumiwa kuachiwa huru,” alisema Dk Hoseah.
Aliwataka wananchi kuwa na imani na chombo hicho katika kushughulikia suala hilo na kwamba haki itatendeka kwa kuwashughulikia watuhumiwa wote kwa haki badala ya kufuata kelele zinazopigwa kwamba hawafanyi kitu au kuwashughulikia watuhumiwa wakubwa.
Tangu kuibuka kwa sakata la kuchotwa kwa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) baada ya kuwepo kwa mgogoro wa kibiashara baina ya Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) na kampuni ya kufua umeme ya IPTL, hatua kadhaa zimechukuliwa na Serikali.
Hizo ni pamoja na kuvunjwa kwa Bodi ya Wakurugenzi Tanesco, kutenguliwa kwa Uwaziri wa Dk Anna Tibaijuka aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, lakini pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alijiuzulu mwishoni mwa mwaka jana, kama ilivyokuwa kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliyejiuzulu mwezi uliopita.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Eliakim Maswi amesimamishwa ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake juu ya ushiriki wake katika sakata hilo lililoteka mkutano wa 16 na 17 wa Bunge ambao uliibuka na maazimio manane, yakiwemo ya kuwawajibisha waliotajwa kuhusika kwa namba moja ama nyingine uchotwaji wa karibu sh bilioni 300 katika akaunti ya Escrow.

No comments: