UMEME KUSHUKA BEI, SUMATRA WAFIKIRIA KUSHUSHA NAULI


Baada ya kushuka kwa bei ya mafuta nchini, wakati wowote kuanzia leo Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) linatarajiwa kutangaza bei mpya za umeme ambazo zitakuwa na unafuu kwa wananchi.

Kutangazwa kwa bei hiyo ni agizo la Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene la kuwataka kuangalia uwezekano wa kushusha gharama za umeme ili kushuka kwa mafuta kuwaguse moja kwa moja wananchi wa kawaida.
Aidha, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) nayo imetakiwa kuangalia namna itakavyoweza kushusha bei za nauli ili kushuka kwa gharama za mafuta, kuendane sambamba na kuwagusa wananchi.
Simbachawene alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam, baada ya mkutano wa pamoja kati ya wadau na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na wizara hiyo.
Alisema, ingawa matumizi ya mafuta katika kuzalisha umeme yamepungua, lakini kwa mitambo na kiasi kinachotumika katika kuzalisha umeme lazima ionekane kushuka kwa bei ya umeme.
"Tanesco waangalie ni kwa kiasi gani gharama za uzalishaji, kwa sababu hizo gharama za uzalishaji wa umeme ndiyo zinazotumika kupanga bei ya umeme.
”Hivyo lazima tuoneshe Ewura wanapotangaza zile bei, aidha imepanda basi kiasi kile ambacho wananchi huwa wanajisikia vibaya sasa wajisikie raha kwamba tunaona bidhaa hii ya mafuta imeshuka bei, kwa hiyo uzalishaji wa umeme nao unashuka gharama yake," alisema.
Alisema ni lazima bei hizo zishuke hata kama ni kwa gharama ndogo kutokana na mitambo mingi inatumia maji na gesi, lakini kiwango hicho ni lazima kionekane kushuka.
Aidha, alisema angependa kuona kila shughuli inayogusa nishati ya mafuta ikiwemo mashine za kusaga zinazotumia nishati hiyo zinashusha gharama zake tofauti na hapo wananchi hawataona kushuka huko na lawama zitaelekezwa kwa serikali.
Akizungumzia kuhusu suala la usafiri, aliiomba Sumatra iweze kuchukua hatua za haraka za kutangaza bei mpya za nauli ambazo zitakuwa chini tofauti na ilivyo sasa.
Awali akijibu maswali na hoja za wadau  hao, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema kusimamishwa kwa ufuatiliaji wa uchakachuaji na wanaokwepa kodi kwa umwagaji wa mafuta ya nje  nchini, itarudisha hali ya miaka ya nyuma, ambapo alisema ni vyema mradi huo ukaendelea kutokana na kuisaidia serikali kukusanya mapato mengi.
Mkutano huo ulikuwa unalenga kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu sekta hiyo, ikiwemo changamoto wanazokumbana nazo.
Tangu kuanza kwa mwaka huu, bei ya bidhaa za petroli zimekuwa zikishuka bei kutokana na kushuka kwa bei katika soko la dunia. Tayari unafuu umeanza kuonekana kwa watumiaji wa petroli, dizeli na mafuta ya taa, bidhaa ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikiuzwa kwa bei ya juu ya Sh 2000, lakini sasa zimeshuka na kuwa chini ya Sh 1,800.
Kutokana na hali hiyo, wadau wamekuwa wakihimiza kuangaliwa kwa uwezekano wa nafuu hiyo ya bei kugusa pia maisha ya kila siku ya mwananchi, ikiwa ni pamoja na kupunguza nauli katika vyombo vya usafiri.

No comments: