Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na
Majini (Sumatra) imeshikwa kigugumizi kuhusu suala la kushusha nauli ya magari
ya abiria kwa kutoa sababu za kisheria pamoja na ukokotoaji wa tozo.
Ikasema, kwa mujibu wa Kanuni za Tozo pamoja
na Sheria, Sumatra inapaswa kurejea tozo ya huduma baada ya mtoa huduma au
mtumiaji wa huduma kupitia Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma
zinazodhibitiwa na Sumatra (Sumatra CCC) kuwasilisha maombi.
Pia huridhia viwango kwa kuzingatia masuala
yote yanayoathiri gharama za uendeshaji, mafuta ikiwa ni moja ya eneo muhimu
katika kukokotoa tozo zinazostahili kuridhiwa.
Meneja Mawasiliano kwa Umma, David Mziray
alisema mwasilishaji wa maombi awe ni mtoa huduma au Sumatra CCC anapaswa atoe
maelezo ya kina kuhusu sababu za kuomba mabadiliko ya tozo, jinsi
alivyoathirika, ikiwa ni pamoja na kuambatisha nyaraka muhimu zinazoweza
kuthibitisha hoja zake.
Alisema maoni ya wadau huzingatiwa kwa pamoja
na masuala yaliyoainishwa katika Sheria ya Sumatra ambayo inatoa muongozo wa
masuala ya kuzingatia katika kuridhia viwango vya tozo mbalimbali.
Alisema masuala hayo ni pamoja na gharama za
uendeshaji, haja ya kukuza ushindani katika soko na kulinda maslahi ya watumia
huduma na watoa huduma.
Akizungumzia kuridhia viwango kwa kuzingatia
masuala yote yanayoathiri gharama za uendeshaji wanazingatia umuhimu wa kuwa na
huduma endelevu, kulinda maslahi ya watumiaji na watoa huduma kwa kuweka
mizania sawa na gharama za uendeshaji ikiwa ni pamoja na mishahara na gharama
za matengenezo.
Pia gharama za vipuri na matairi, gharama
zaununuzi wa mabasi, riba kutokana na mikopo, gharama za bima, mafuta
navilainishi, gharama nyingine za kiutawala, kodi na tozo mbalimbali, athari za
viashiria vya kiuchumi kama mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya shilingi
na kujenga mazingira ya ushindani.
Mziray alisema lengo la Sumatra katika kupanga
nauli ni kuona pamoja na mambo mengine kuwa katika viwango vinavyoridhiwa kuna
kuwa na ushindani zaidi miongoni mwa watoa huduma na hivyo kuwa na huduma bora
zaidi na endelevu.
“Ni vyema kutambua kuwa kwa kiasi kikubwa
huduma za usafiri wa umma zinatolewa na sekta binafsi, wengi wao wenye kipato
cha kawaida. Hivyo basi nauli inayolipwa na abiria ndiyo inayolipia gharama za
uendeshaji na kumpa mtoa huduma uwezo ili huduma iwe endelevu na kuvutia
wawekezaji zaidi kuingia katika biashara hiyo,” alisema.
Alisema katika mazingira ambayo watoa huduma
wamekuwa wakijielekeza katika kupata faida iliyokithiri, Sumatra imekuwa na
jukumu la kuhakikisha kuwa mtumia huduma analindwa dhidi ya nauli kubwa kupita
kiasi ambayo inaweza kumfanya mtumiaji
huduma kushindwa kutumia huduma hiyo.
No comments:
Post a Comment