Baadhi ya wakazi wa jijini Tanga wamepongeza hatua
ya awali iliyofikiwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na JWTZ kwenye
operesheni maalumu ya kusaka wahalifu pamoja na silaha waliokuwa wamejifisha
katika mapango ya Majimoto yaliyopo eneo la Mzizima Amboni, nje kidogo ya mji.
Pongezi hizo zilitolewa jijini hapa jana na wakazi
mbalimbali baada ya kupatikana kwa bunduki ya SMG yenye risasi 20, mhalifu
pamoja na watu wengine wanaoendelea kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo.
Walisema hatua hiyo ni mwanzo wa mafanikio ingawa
wakaongeza kwamba jitihada zaidi zinapaswa kuongezwa ili kuhakikisha silaha na
vitu vingine vyote vinapatikana kwa wakati kabla ya kuleta madhara kwa jamii.
Mwajuma Msagati, mkazi wa Chumbageni alisema
taarifa ya jana ya Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul
Chagonja alivyonukuliwa kwenye vyombo vya habari imeendelea kupunguza wasiwasi
kwenye jamii.
“Unajua tetesi na taarifa zimekuwa nyingi kiasi
kwamba huelewi ushike ipi au amuamini nani lakini kwa kweli taarifa kuhusu
tatizo hilo ambazo zimeanza kutolewa wiki hii na Mkuu wa Mkoa wa Tanga pamoja
na Jeshi la Polisi zimetupa matumaini mapya ya kuanza kuimarika kwa hali ya
amani,” alisema.
Naye Peter Mgembe, mkazi wa Mafuriko Amboni alisema
hali ya ulinzi na usalama iko shwari ingawa magari yenye vikosi vya askari
yamekuwa yakipita pita kuelekea eneo tukio.
“Kwa kweli hata upitaji wa magari yenye askari sio
ule wa kutisha kama ilivyokuwa mwishoni mwa wiki… kwa sasa wanaonekana kama
wanafanya doria za kawaida …kwa hali hii tunayoiona sasa imeturejeshea tumaini la
kuwepo kwa amani na tunapata ujasiri wa kuweza kuendelea na shughuli zetu za
uzalishaji kama awali”, alisema.
No comments:
Post a Comment