SERIKALI YASOMESHA WAHADHIRI 398


Wahadhiri  398 wamesomeshwa na serikali ndani ya miaka mitano ikiwa ni mkakati wa kuongeza wanataaluma hao ili idadi iendane na ongezeko la vyuo na wanafunzi.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufunzi, Dk Shukuru Kawambwa alitoa taarifa hiyo mwishoni mwa wiki katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (Muce) alipokuwa akielezea utekelezaji wa Mradi wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu (STHEP). 
Alisema wahadhiri hao  wamesoma katika vyuo mbalimbali nchini na nje ya nchi chini ya utekelezaji wa mradi  huo. Kati yao,  188 walidahiliwa katika Shahada ya Uzamivu na 208 ni wa Shahada za Uzamili.
“Kwa wale waliodahiliwa katika Shahada ya Uzamivu, watumishi 57 ambao ni asilimia 30 ni wanawake na wale wa Shahada ya Uzamili wanawake ni asilimia 21 (watumishi 44),” alisema.
Aliongeza kwamba, wanataaluma 203 walikuwa wamehitimu mafunzo yao na 195 wakiwa katika hatua za mwisho.
Kawambwa alisema mradi huo pia umegharimia ujenzi wa majengo mapya 25, ikiwa ni pamoja na kuyafanyia ukarabati yaliyokuwepo katika vyuo vikuu saba vilivyo katika mradi huo ambayo yatatumiwa na wanafunzi 47,622 nchini kote.
Majengo hayo pia yana jumla ya vyumba vya ofisi 1,794 kwa ajili ya wahadhiri, wakufunzi, wakutubi, wataalamu wa maabara na wengine.
Akizungumzia mipango ya baadaye baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza ya STHEP, Kawambwa alisema wizara yake imeanza kutekeleza mradi mpya kwa mkopo nafuu wa Benki ya Dunia ambao utadumu kwa miezi 18.
Alisema mradi huo utatumika kukamilisha miundombinu na majengo yaliyokumbwa na ukosefu wa fedha katika mradi wa kwanza yakiwamo majengo ya kufundishia yaliyokosa samani, umeme na pia uunganishwaji wa taasisi nane kwenye mkongo wa taifa.
Waziri Kawambwa alisema mradi huo pia utasaidia kufanya tafiti kuhusu mahitaji ya utaalamu na maarifa nchini na kuandaa mradi wa STHEP awamu ya pili.

No comments: