Idadi ya wagonjwa wa saratani katika Hospitali
ya Rufaa ya Bugando jijini, Mwanza imeongezeka kutoka 3,400 mwaka 2009
hadi kufikia wagonjwa 10,200 mwaka jana.
Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Idara ya
Saratani, Dk Nestory Masalu wakati akitoa taarifa juu ya hali ya maendeleo ya ugonjwa huo
katika hospitali hiyo.
Alisema ongezeko hilo linachangiwa na huduma
za uchunguzi nje ya kituo, uchunguzi wa awali ndani ya kituo, elimu na
mazingira ambayo ni pamoja na Ziwa Victoria, shughuli za migodi na virusi vya
Ukimwi.
Alisema kati ya asilimia 70 na 80 ya
wagonjwa wa saratani wanaofika hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu huwa katika hatua ya mwisho ya ugonjwa ambayo
husababisha matokeo ya matibabu yake yasiwe mazuri.
Dk Masalu alisema asilimia 30 ya watu wazima
na asilimia 50 ya watoto hupona baada ya kukamilisha matibabu, lakini wengi wao
huhitaji tiba shufaa.
Alisema wagonjwa 400 wamenufaika na huduma ya
kipimo ambacho huwawezea kujua saratani
imefikia wapi, kwa kiwango gani tangu mwaka 2011 kilipoanza kufanya kazi.
Dk Masalu
alisema kwa ushirikiano wa Wataliano waliweza kufanya huduma nje ya
hospitali katika kuchunguza saratani ya matiti na shingo ya kizazi ambapo akina
mama 4,000 wamechunguzwa kwenye vituo mbalimbali.
Alisema kwa sasa Tanzania imekuwa ikiwaona
wagonjwa 600,000 ambapo idadi hiyo itaongezeka ifikapo mwaka 2030 ambapo
wagonjwa zaidi ya 800,000 wapya watapatikana.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa BMC, Profesa Kien Mteta alisema saratani ni ugonjwa wa
vinasaba katika mwili wa binadamu ambapo hukosea kutengeneza seli za binadamu.
No comments:
Post a Comment