AFUNGWA JELA MAISHA KWA KUMBAKA MTOTO WA MIAKA MITANO


Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Nzega mkoani Tabora imemhukumu kifungo cha maisha  Kashindje Shija (50), baada ya kupatikana na kosa la kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka mitano.

Akisoma hukumu hiyo mwishoni mwa wiki,  Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Nzega Joseph Ngomero, alisema kuwa, kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, amelazimika kutoa hukumu hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaokusudia kufanya vitendo kama hivyo.
Hakimu Ngomero aliongeza kwa kusema kuwa, kutokana na kitendo cha kinyama alichokifanya Shija cha kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 5, mahakama hiyo imelazimika kumhukumu kifungo cha maisha jela.
Awali Mwendesha Mashitaka wa Serikali wilayani Nzega Melito Ukongoji aliiambia mahakama hiyo kuwa, mnamo Mei 19, 2014 katika  Kijiji cha Kidete wilayani Nzega  saa 8 mchana, Shija alifumaniwa chini ya mti wa mwembe akiwa anambaka mtoto huyo.
Aidha Melito aliongeza kuwa kutokana na kitendo alichokifanya mtuhumiwa
kilimsababishia mtoto huyo maumivu makali katika mwili wake  pamoja na kutoka damu nyingi.
Mwendesha Mashitaka huyo, aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo  kutokana na kitendo kilichofanywa na mtuhumiwa cha kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 5.
Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, mahakama hiyo ilitoa nafasi ya utetezi kwa mtuhumiwa ambapo aliiomba mahakama hiyo kumpunguzia adhabu kutokana na kuwa mwathirika wa virusi vya Ukimwi.

No comments: