SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA ZANZIBAR YAICHEFUA CCM


Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema hakitaunda tena Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kutokana na  baadhi ya washiriki wake kuvuruga utaratibu na misingi ya kuanzishwa kwa serikali hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi Zanzibar, Waride Bakari Jabu  wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika  Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini hapa Zanzibar.
Waride alisema makubaliano yanayotokana na kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa sasa yameanza kuvurugwa na kukiukwa kidogo kidogo katika misingi yake mikuu huku kauli za chuki na uhasama zikitawala.
Alikumbusha viongozi wa vyama vya siasa kwamba sababu za kuwapo  kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni tofauti za kisiasa  na   kauli za chuki  ambazo zilisababisha kuwepo kwa malumbano ya kisiasa katika majukwaa ya kisiasa.
Alisema kwa bahati mbaya, misingi hiyo sasa imeanza kuyumba na kuporomoka kidogo huku matusi na kejeli kwa viongozi wakuu wa serikali akiwemo Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, zikichukua nafasi kubwa.
“Chama Cha Mapinduzi kimesikitishwa sana na kauli za chuki na uhasama, zinazotolewa na  Makamo wa Kwanza wa Rais  Maalim Seif Sharif Hamad  ambazo zinaashiria kuyumba kwa serikali ya umoja wa kitaifa na kurudisha chuki na uhasama,” alisema.
Waride alifafanua kwamba CCM  ambayo ni mshirika anayeunda  Serikali ya Umoja wa Kitaifa, inatamka bayana kwamba haipo tayari kushiriki kuunda serikali hiyo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Alifahamisha CCM haikuwa na sababu ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa sababu ilipata ushindi wa kutosha, uliowafanya kuunda serikali. Hata hivyo ilifanya hivyo kwa ajili ya kukidhi matakwa ya sheria.
“CCM haioni sababu tena ya kuwepo kwa serikali ya umoja wa kitaifa kwa sababu wenzetu CUF wamekuwa wakitoa kauli za chuki na uhasama zinazorudisha nyuma matarajio ya wananchi wa kuwepo maridhiano ya kisiasa,” alisema.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliundwa kisheria mwaka 2010 baada ya vyama vikuu vya siasa visiwani hapa, CCM na CUF, kujadiliana na hatimaye kufikia mwafaka wa kugawana madaraka, kuondoa siasa za chuki, zilizotokana na machafuko ya mwaka 2005 wakati wananchi walipokuwa wakipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Rais.
Katika hatua nyingine, Kamati Kuu ya CCM itakutana Jumamosi ijayo kujadili mambo mbalimbali.
 Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, ilieleza kuwa vikao vingine muhimu vya chama hicho, vinaendelea kufanyika kwa ajili ya kikao hicho cha juu.

No comments: