RITA YAANZA KUTOA VYETI VYA KUZALIWA KINONDONI


Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), unategemea kuanza rasmi mkakati wa kuwasajili na kuwapa vyeti vya kuzaliwa wanafunzi wa shule za msingi za Manispaa ya Kinondoni na mpango huo utatekelezwa katika takribani shule 140 zenye wanafunzi wapatao 155,944.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kitengo cha mawasiliano cha wakala huyo, lengo la usajili huo katika awamu hiyo ni kusajili wanafunzi 20,000.
Ilisema kuzinduliwa kwa mkakati huo katika Manispaa ya Kinondoni ni muendelezo wa mkakati mkuu uliozinduliwa Aprili, mwaka jana unaowawezesha wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari kusajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa katika shule wanazosoma.
Taarifa ilisema baada ya mwalimu kuwatangazia wanafunzi na wazazi kuhusu huduma hiyo kupatikana shuleni atagawa fomu za maombi kwa wanaohitaji, kuhakiki fomu zilizojazwa, kuzikusanya na kuziwasilisha  RITA kwa ajili ya kuhakiki na kuandaliwa vyeti.
Tayari mkakati huo umeshaanza kutekelezwa katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam na umeshafanyika katika shule 105 za msingi na 96 za sekondari za Manispaa ya Ilala na kuonesha mafanikio ambapo zaidi ya wanafunzi 16,000 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.

No comments: