PAPAA MSOFE ASHINDWA KUTOKEA MAHAKAMANI


Mfanyabiashara mashuhuri, Marijan Abubakar maarufu kama Papaa Msofe (50) anayekabiliwa na kesi ya mauaji, ameshindwa kufika mahakamani kwa kuwa anaumwa.

Kesi hiyo ilitajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu lakini Wakili wa Serikali Hellen Moshi alidai bado upelelezi haujakamilika na kwamba Papaa Msofe hakufika  mahakamani, kwa kuwa wamepata taarifa kuwa anaumwa.
Hakimu Mkazi Hellen Riwa aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 5, mwaka huu itakapotajwa tena kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi umekamilika.
Msofe ambaye kwa mara ya kwanza alifikishwa mahakamani hapo Agosti 10, mwaka 2012  anadaiwa Novemba 6,  mwaka 2011 katika eneo la  Magomeni Mapipa, yeye na mwenzake  Makongoro Nyerere, kwa kukusudia walimuua Onesphory Kitoli.
Washitakiwa wanaendelea kusota rumande kwa kuwa kesi inayowakabili kisheria haina dhamana.

No comments: