NDEGEVITA YA JWTZ YAANGUKA NA KUTEKETEA MWANZA


Ndegevita ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),  iliyokuwa katika mazoezi, imeanguka na kuteketea moto huku rubani wake akiumia wakati akijiokoa katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Taarifa hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya jeshi hilo. Ilieleza kuwa ndege hiyo iliwaka moto baada ya ndege (mnyama) kuingia ndani ya injini moja wakati ndege ikiruka.
Naibu Mkurugenzi wa kurugenzi hiyo, Meja Joseph Masanja akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Jeshi hilo aliwataka wananchi wasipate hofu ndege hiyo imeungua moto katika ajali ya kawaida.
Alisema ajali hiyo ilitokea jana mchana katika uwanja wa ndege wa kijeshi wa Mwanza wakati ndegevita za jeshi hilo zikifanya mazoezi ya kuruka.
Alisema ndege hiyo ya vita ilikuwa ikiendeshwa na rubani Meja Peter Lyamunda ambaye alipoona ndege yake ikiwaka moto aliruka kwa kutumia vifaa maalum hivyo hakupata majeraha makubwa zaidi ya kuumia mguu.
Meja Masanja alisema kwa sasa rubani huyo anaendelea vizuri na kwamba eneo ambalo ndege iliangukia hakukuwa na madhara yoyote.
"Tumetoa taarifa hii kama Jeshi ili wananchi wapate taarifa sahihi, wasipotoshwe ndege hiyo imeanguka na kuungua moto baada ya ndege mnyama kuingia ndani ya injini moja," alisema Meja Masanja.
Alisema wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida ndege hiyo ilikuwa katika mazoezi ya kawaida pamoja na ndege nyingine.

No comments: