Kobe wadogo 250, wamekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Abeid Amani Karume, wakiwa njiani kusafirishwa kwa njia ya magendo
kwenda Malaysia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkadam
Khamis Mkadam, alisema kobe hao walikamatwa wakiwa wamehifadhiwa katika
masanduku yaliyowekwa maembe ndani yake, katika hatua za mwisho za
kusafirishwa.
“Ni kweli tumekamata kobe 250 wakiwa wamehifadhiwa vizuri
katika masanduku yakiwa yameingizwa maembe tayari kusafirishwa kwenda
Malaysia,” alisema.
Hata hivyo Kamanda Hamdani alikataa kumtaja mtu aliyekamatwa
na kobe hao kwa madai kwamba uchunguzi unaendelea na kitendo cha kumtaja moja
kwa moja, kinaweza kuharibu uchunguzi wa tukio hilo.
“Jeshi la Polisi kwa sasa halipo tayari kumtaja mtuhumiwa
aliyekamatwa na kobe hao kwa sababu uchunguzi zaidi unaendelea...unajuwa
ukianza kumtaja mtuhumiwa pamoja na watu wengine, unaharibu uchunguzi mzima wa
tukio hilo,” alisema.
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na matukio ya wizi wa
kobe kutoka Zanzibar kupelekwa sehemu nyingine duniani ikiwa ni pamoja na
Tanzania Bara.
Kobe hao wanalindwa na sheria za kimataifa, wakiwa katika
orodha ya viumbe ambao wapo katika hatari ya kutoweka duniani, kama ilivyo kwa
kasa kwa hivyo wamekuwa katika udhibiti mkubwa.
Kwa upande wa Zanzibar, kobe wanahifadhiwa katika kisiwa
kidogo cha Chumbe kilichopo nje ya Bandari ya Malindi umbali wa kilometa 40,
ambapo hata hivyo kumekuwepo matukio ya wizi wa mara kwa mara.
Ofisa mmoja kutoka Kamisheni ya Utalii Zanzibar, ambaye moja
ya majukumu yake ni kulinda na kuhifadhi kobe waliopo katika kisiwa kidogo
cha Changuu, alikiri kuwepo wizi katika
nyakati tofauti, unaofanywa na watu wasiokuwa waaminifu wanaotembelea kisiwa
hicho kwa shughuli za utalii.
“Yapo matukio ya wizi wa kobe katika kisiwa cha Changuu kwa
nyakati tofauti, kwani watu hufika katika kisiwa kwa shughuli tofauti ikiwemo
za matembezi ya utalii,” alisema.
Katika miaka kumi iliyopita, zaidi ya kobe 1,500 wameibwa
katika kisiwa cha Changuu, wakiwemo kobe wadogo ambao huhifadhiwa katika sehemu
maalumu.
No comments:
Post a Comment