Kivuko cha Mv Dar es Salaam,
kinachotarajiwa kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria kutoka Dar es Salaam
kwenda Bagamoyo, jana kilifanyiwa majaribio ya safari ambapo kilitumia saa
tatu, huku ikielezwa kwamba kitakapoanza kutoa huduma kitatumia saa mbili kwa
safari moja.
Akizungumza katika ziara ya
ukaguzi wa Kivuko hicho, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alisema
wamekifanyia majaribio ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mwisho.
Baada ya majaribio hayo kwa
mujibu wa Dk Magufuli, wanatarajia ndani ya siku 15 watakuwa wamekamilisha
taratibu zote, ambapo kitazinduliwa na Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya kuanza
huduma.
Alisema kivuko hicho
kilichotengenezwa na kampuni ya Johs Gram Hansen ya Denmark, kitakuwa na vituo
saba hadi kufika Bagamoyo na kinatarajiwa kupunguza msongamano mkubwa na adha
ya usafiri kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.
Vituo hivyo kwa mujibu wa
taarifa za Wizara hiyo ni Magogoni, Kawe, Jangwani Beach, Rungwe Oceanic,
Mbweni, Kaole na Mbegani.
Aidha Dk Magufuli alisema watahakikisha
wanaendelea kuwapa kazi Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kamandi
ya Maji, kutokana na utendaji wao mzuri hasa katika ukarabati wa vivuko na
ujenzi wa gati.
"Nawahakikishieni kwamba
tutaendelea kuwapa kazi Jeshi kutokana na utendaji wenu, ingawa najua maneno
haya yanaweza yasiwafurahishe Wakala wa Ufundi na Umene(Temesa), ila ukweli
ndiyo huo," alisema.
Aidha aliwahakikisha wananchi
wa kigamboni kwamba usafiri utaendelea kuimarika, ambapo pia imetengwa Sh
bilioni tatu katika bajeti, kwa ajili ya ununuzi wa kivuko kingine huku ujenzi
wa daraja ukiendelea.
"Tutaendelea kuimarisha
usafiri wa majini ili kupunguza msongamano na foleni katika barabara...
Tunawashukuru sana wananchi kwa kuendelea kuvumilia matatizo madogo madogo ya
usafiri, nawaahidi tutaendelea kutoa ushirikiano, ili kuhakikisha matatizo hayo
yanaisha," alisema.
Dk Magufuli alisema kivuko
hicho kina vifaa vya kisasa, ikiwemo uwezo wa kuona jiwe au mlima hata wakati
wa usiku na kina mwendo wa kasi.
Kuhusu nauli, Dk Magufuli
alisema kitakapoanza kutoa huduma, watapanga nauli nafuu ambayo kila mwananchi
ataimudu, ili atakayetumia kivuko hicho aone nafuu kuliko kupanda daladala.
Naye Mtendaji Mkuu wa Temesa,
Marycelina Magesa, alisema kivuko hicho kimetengenezwa kwa fedha za Serikali
kwa asilimia 100 na kimegharimu Sh bilioni 7.9 na kinauwezo wa kubeba abiria
300.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Raymond Mushi alisema kivuko hicho kitasaidia kuinua shughuli za
wananchi wa mkoa huo na Pwani kwa kupunguza foleni, ambazo zimekuwa zikipoteza
muda mwingi barabarani.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa
wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema kivuko hicho kimekuja muda muafaka hasa
katika Mkoa huo, kwa kuwa Bagamoyo ni eneo la Ukanda wa Kiuchumi na utakuwa mji
wa uwekezaji mkubwa kuanzia Julai mwaka huu.
Aidha aliomba Wizara hiyo
kuboresha miundombinu hasa upande wa Bagamoyo, ili iwe rahisi kwa wananchi kwa
kuwa kwa sasa hali watalazimika kupanda magari mawili ili kufika kwenye kivuko.
"Naomba miundombinu
iboreshwe na pawe na usafiri wa moja kwa moja hadi mjini kwa sababu kwa sasa
mtu akitoka mjini, analazimika kushuka Zinga ndiyo aje hapa Mbegani kupanda
kivuko ila ukiwepo usafiri wa moja kwa moja utasaidia sana," alisema.
Katika
ziara hiyo, Magufuli alisafiri hadi Bagamoyo na viongozi mbalimbali wa Serikali
wakiwemo kutoka wizara hiyo, Temesa, Wakala wa Barabara (Tanroad), JWTZ Kamandi
ya Maji na wananchi ambao walipata fursa ya kwenda Bagamoyo na kurudi bila
malipo.
No comments:
Post a Comment