HATIMA YA WANAOSAKA URAIS WA CCM LEO

Kamati Kuu ya CCM (CC) iliyosubiriwa kwa muda mrefu, hatimaye inakutana leo na suala kubwa linalotarajiwa na wanachama na wananchi, ni tathmini ya hukumu ya vigogo sita wa chama, waliokuwa wakitumikia adhabu baada ya kubainika kuanza kampeni za urais mapema.

Vigogo ambao tathmini ya mwenendo wao inasubiriwa baada ya kikao hicho ni pamoja na waliokuwa mawaziri wakuu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ambaye ameshatangaza nia ya kugombea urais, Waziri wa Kilimo na Ushirika, Stephen Wassira na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Mwanzoni mwa wiki hii, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari, ikielezea kuwepo kwa kikao cha Kamati Kuu leo kitakachoongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
Ingawa ajenda za kikao hicho hazikuwekwa wazi, lakini tayari duru za siasa na wachambuzi mbalimbali, walishaanza kuzungumzia umuhimu wa ajenda ya tathmini ya hukumu ya makada hao, kwa kuwa muda wa kutumikia adhabu hiyo ya mwaka mzima ulikamilika katikati ya mwezi huu.
Vigogo hao wanaotajwa kutaka kuwania urais, walipewa adhabu hiyo ya onyo kali na Kamati Kuu Februari 18, mwaka jana baada ya kuthibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati, kinyume na kanuni za uongozi na maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7) (i).
Vilevile baada ya kuhojiwa, walithibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii.
Kutokana na adhabu ya onyo kali, vigogo hao kwa mwaka mzima walikuwa katika hali ya kuchunguzwa, ili kuwasaidia katika jitihada za kujirekebisha.
Pia kamati ndogo ya udhibiti iliagizwa kuchunguza na kuchukua hatua kwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine, katika vitendo hivyo vilivyovunja kanuni za chama.
Moja ya vitu vinavyosababisha wachambuzi wa siasa kuamini umuhimu wa ajenda hiyo katika kikao cha leo, ni tamko la chama hicho lililotolewa Januari mwaka huu, baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu.
Katika tamko hilo, CCM iliweka wazi kuwa baada ya kukamilika kwa adhabu hiyo, Kamati Kuu ndio kikao ambacho kingefanya tathmini ya utekelezaji wa adhabu hiyo kwa vigogo hao.
Tamko hilo lilienda mbali zaidi na kubainisha kuwa, vigogo ambao watabainika katika kikao hicho cha tathmini,  kuwa walikiuka masharti ya adhabu hiyo, adhabu zao zingeongezwa.
Kabla ya kuhukumiwa kutojihusisha na masuala ya kampeni kwa mwaka mmoja,  Kamati ya Maadili ya CCM, inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, iliwahoji watuhumiwa hao.
Miongoni mwa wajumbe walioshiriki kuhoji watuhumiwa hao mbali na Mangula, alikuwepo Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana, William Lukuvi ambaye ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Shamsi Vuai Nahodha, ambaye alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.  
Ajenda nyingine inayotarajiwa kunguruma katika kikao hicho ni kuhusu vigogo wa chama hicho, waliokumbwa na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kikao cha Kamati Kuu ya CCM cha Januari kilichoketi Zanzibar, kilieleza kusikitishwa kwake na baadhi ya viongozi wake walio katika dhamana ya kisiasa kukumbwa na kashfa hiyo.
Aidha, kiliagiza Kamati ya Maadili kuchukua hatua za kimaadili kwa wale wote waliohusika na ukiukaji wa maadili kwenye sakata la Escrow, ambao wako kwenye vikao vya uamuzi vya chama.
Wanaotuhumiwa na kukiuka maadili katika fedha hizo ni pamoja na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, Ngeleja na Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Mwingine katika tuhuma hizo, ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

No comments: