MWANASHERIA WA TANESCO ABADILISHIWA KESI ESCROW


Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco, Steven Urassa amefutiwa mashitaka ya kupokea sehemu ya fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow na kusomewa mashitaka ya kupokea rushwa ya Sh milioni 161.7.

Urassa aliondolewa mashitaka hayo baada ya Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai kubadilisha hati ya mashitaka dhidi yake.
Akisoma hati hiyo mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda, Swai alidai Februari 14, 2014 katika eneo la Benki ya Mkombozi, Urassa akiwa Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco alipokea rushwa ya Sh 161,700,000 kupitia akaunti namba 00120102658101.
Alidai Urassa alipokea fedha hizo kutoka kwa Mshauri wa Kimataifa ambaye ni Mkurugenzi wa VIP Engineering na Mkurugenzi wa zamani wa IPTL, James Rugemalira kama tuzo hiyo baada ya kuiwakilisha Tanesco na IPTL katika kesi ya Standard Charter nchini Hong Kong.
Aliendelea kudai kuwa Urassa alipokea fedha hizo bila kutangaza maslahi kwa bosi wake ambaye ni Meneja wa Tanesco.
Upelelezi wa kesi umekamilika lakini upande wa utetezi ulidai kuna masuala ya kikatiba yanajitokeza katika kesi hiyo ambayo yanatakiwa kusikilizwa katika Mahakama Kuu. Waliiomba mahakama isikilize hoja zao na kuzitolea maelekezo kabla ya kuendelea na usikilizwaji wa kesi.
Hakimu Kaluyenda aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 17 mwaka huu kwa ajili ya kusikiliza pingamizi la upande wa utetezi.
Awali Urassa alikuwa anakabiliwa na mashitaka ya kupokea fedha hizo ambazo ni sehemu ya fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.

No comments: