TBS WATEKETEZA JUISI ISIYO NA VIWANGO


Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeteketeza tani saba za juisi ya U-Fresh inayozalishwa na Kiwanda cha U-Fresh  Food Limited ya Tegeta, Dar es Salaam kwa sababu ya kukosa viwango vya ubora vinavyotakiwa.

Juisi hizo, ambazo ni katoni 1,400, ziliteketezwa katika dampo la Pugu, nje kidogo ya Dar es Salaam, kwa gharama za wamiliki wa kiwanda hicho, ambao ni raia wa China. Katoni moja inauzwa Sh 4,000.
Akizungumza wakati wa uteketezaji wa juisi hizo ulioshuhudiwa na Mkaguzi wa Viwango vya Bidhaa wa TBS, Inspekta Edimitha Protace, Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano cha shirika hilo, Roida Andusamile alisema, tani hizo za juisi zilizoteketezwa zimekusanywa na mzalishaji mwenyewe kutoka sokoni.
"Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdalla Kigoda, aliwaagiza wazalishaji wote waliozuiwa kuendeleza uzalishaji nchini kwa sababu bidhaa zao hazikidhi matakwa ya viwango vya ubora vya kitaifa na kimataifa, waziondoe sokoni ndani ya siku 14 zilizoanza Januari 28 na kuisha kesho (leo)".
"Kwa asilimia kubwa, wazalishaji hao wametekeleza agizo la Waziri, na sisi kama shirika tunajipanga kuingia sokoni kufanya ukaguzi wa siri, kuhakikisha endapo zimeondolewa zote kutoka katika masoko mbalimbali nchini, kwa sababu tuna orodha ya wazalishaji hao. Lengo letu ni kujiridhisha kuwa walaji wanapata bidhaa bora na si bora bidhaa," Andusamile alisema.  
Kwa upande wake, Meneja Masoko wa U-Fresh, Kephas Gembe alisema, wanakiri kuwa juisi yao haikuwa bora na kwamba maelekezo yote waliyopewa na TBS kwa ajili ya kurekebisha kasoro zilizoonekana wameyatekeleza na kuliomba shirika hilo liwakague upya ili waendeleze uzalishaji.
Kwa mujibu wa Gembe, kuanzia Desemba 24, mwaka jana, walipozuiwa kuendeleza uzalishaji walikuwa wakiwasiliana na wateja wao ili wasimamishe uuzaji.
"Hata tangazo la waziri lilipotolewa tayari tulikuwa tumeanza kuzikusanya. Jana pia (juzi) tuliutangazia umma utuletee taarifa ya wanaoendelea kuziuza ili tukaziondoe madukani mwao. Wauzaji ambao hatujawafikia kuzichukua nao tumewaomba wazirudishe kiwandani ili tufanye utaratibu wa kuziteketeza," alisema.   
Akijibu ni kwa nini zilizofikishwa dampo ili kuteketezwa zilikuwa kidogo zaidi ya zilizokutwa kiwandani wakati wa ukaguzi wa kushtukiza, Meneja Masoko huyo alisema, kiasi hicho ndicho kilichokusanywa kutoka sokoni na kwamba zilizofungiwa kiwandani na TBS hazijateketezwa,kwa sababu hawana ruhusa ya kuzigusa hadi shirika hilo lisimamie utoaji wake kujiridhisha kuwa zipo kama zilivyokuwa zimefungiwa.

No comments: