MWAKILISHI KWA TIKETI YA CCM AFARIKI DUNIA GHAFLA


Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni kwa tiketi ya (CCM), Salmin Awadh Salmin (57) amefariki ghafla akiwa katika eneo la Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui ambapo alikuwa katika shughuli zake za kawaida za kichama.

Kwa mujibu wa taarifa za baadhi ya wajumbe waliohudhuria kikao hicho, alikuwa akizungumza na baadhi ya wajumbe wenzake wa Baraza la Wawakilishi ndipo ghafla alianguka na  kufa papo hapo.
“Sisi tunamaliza kikao cha Sekretarieti tunapewa taarifa kwamba ameanguka na ndipo alipofikishwa haraka katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na kufariki'alisema Khadija Hassan Aboud, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM ambaye alikuwa pamoja na Salmin.
Wakati huohuo, Jakaya Kikwete amempelekea Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha mbunge huyo.
Salmin alikuwa pia Katibu wa Kamati ya Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Baraza la Wawakilishi.
Katika salamu zake, Rais Kikwete alisema: “Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Salmin Awadh Salmin, Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni katika Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Baraza hilo ambaye nimejulishwa ameanguka ghafla wakati akihudhuria kikao mjini Zanzibar.”
“Nakutumia Mheshimiwa Rais salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo hiki kikubwa. Aidha kupitia kwako, nawatumia salamu za rambirambi wananchi wa Magomeni ambao wamepoteza Mwakilishi wao na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliopoteza mwenzao na kiongozi wao.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Kupitia kwako,vile vile, natuma pole nyingi sana kwa familia, ndugu na jamaa wa Mheshimiwa Salmin kwa kuondokewa na mhimili mkuu wa familia na mlezi. Wajulishe niko nao katika msiba huu mkubwa na kuwa msiba wao ni msiba wangu pia. Napenda pia uwajulishe kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema roho ya marehemu.”

No comments: