AJALI YA BASI YAUA ABIRIA WAWILI NA KUJERUHI WENGINE 45


Watu wawili wamekufa papo hapo huku wengine 45 wakijeruhiwa baada ya basi la abiria lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mwanza kugongana uso kwa uso na lori katika kijiji cha Vikonje wilayani Chamwino mkoani hapa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema kuwa ajali hiyo ilitokea saa 7.05 mchana wakati basi la Kidia lenye namba za usajili T663 AXL kugonga lori lenye namba za usajili T 496 CFG na trela lenye namba za usajili T576 AZX Scania.
Alisema basi hilo lilikuwa likitokea  Dar es Salaam kwenda Mwanza wakati lori lilikuwa likitokea Dodoma kwenda  Dar es Salaam.
Aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni dereva wa lori, Fadhili Said (36) na utingo wa basi, Chogo Chigunda.
Kamanda Misime alisema ajali hilo ilitokea wakati dereva wa basi la Kidia, Adam Robert (34) alipokuwa akilifuata gari lililokuwa likilipita gari la mbele yake.
Alisema dereva wa basi baada ya kushindwa kulipita gari lililo mbele yake alikutana na lori lililokuwa likija mbele yake na kusababisha ajali hiyo.
Alisema Jeshi la Polisi wanamfuatilia dereva wa basi ambaye anatibiwa majeraha katika moja ya hospitali mjini hapa.
Pia alisema majeruhi hao bado walikuwa wakitibiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na wengine wameruhusiwa kurejea nyumbani.

No comments: