MIKOA SITA TAABANI KATIKA UJENZI WA MAABARA


Mikoa sita 'imevurunda' katika ujenzi wa maabara katika shule za sekondari baada ya kushindwa kufikia malengo. Ni mikoa mitatu pekee ndiyo imefanya vizuri kwa kuvuka nusu ya malengo.  
 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alitaja mikoa ambayo haikufika hata robo ya malengo kuwa ni  Mtwara (asilimia 21), Lindi (asilimia 20), Tabora (asilimia 17), Dodoma (asilimia 12), Rukwa (asilimia 11) na Kigoma (asilimia 10). 
“Tunaweza kusema hii ndiyo mikoa ya mwisho katika kutekeleza agizo la Rais.  Mikoa 16 ambayo sikuitaja hapa iko katika kundi la asilimia kati ya 26 hadi 49,” alisema Pinda kupitia hotuba yake ya kuahirisha Bunge la 18.  
Pinda alitaja mikoa mitatu iliyofanya vizuri kuwa ni Njombe uliofanikiwa kukamilisha ujenzi kwa asilimia 96 wa maabara za shule za sekondari, Ruvuma iliyokamilisha kwa asilimia 81 na Morogoro ambao ni watatu kwa kujenga vyumba kwa asilimia 53.   
Waziri Mkuu alipongeza Ruvuma na Njombe kwa kutekeleza vizuri maelekezo ya Rais, akisema imeonesha mfano mzuri. Alisema  Morogoro ni wa tatu. Alisema Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake kwa wananchi, Desemba 31 mwaka jana, aliongeza miezi sita zaidi hadi Juni 2015 kwa ambao hawajakamilisha ujenzi wa maabara hizo, ili wakamilishe.  
Pinda alisema matarajio ya Rais Kikwete ni kwamba muda huo unatosha kwa kila sekondari nchini kuwa na vyumba vitatu vya maabara .
“Hivyo, ninawataka wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, mameya, wenyeviti na wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya na miji nchini kuhakikisha maagizo haya yanatekelezwa. Aidha, ninatoa rai kwa waheshimiwa wabunge na madiwani kutoa msukumo stahiki katika utekelezaji wa maagizo haya kwa maslahi ya Taifa letu,” alisema.
Kwa upande wa Serikali, Pinda alisema Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), haina budi kuhakikisha agizo linatekelezwa ndani ya muda uliotolewa; yaani Juni mwaka huu.
Aidha, alisisitiza katika usimamizi, Tamisemi ihakikishe  vyumba vya maabara vinavyojengwa vinakuwa na ubora stahiki na vinalingana na thamani ya fedha zilizotumika.  
Amesema ubadhirifu wa aina yoyote usipewe nafasi na watakaobainika kuhusika wachukuliwe hatua za kisheria mapema.
“Nitapenda Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi waendelee kufuatilia suala hili na kunipa taarifa mara kwa mara,” alisema.  
Mwaka 2012, Rais Kikwete akiwa ziarani katika mkoa wa Singida, alielekeza kila shule ya sekondari nchini iwe ina vyumba vitatu vya maabara ifikapo Novemba 30,  2014.
Tangu wakati huo hadi sasa, utekelezaji unaendelea na kwa mujibu wa Waziri Mkuu, hali ya ujenzi wa vyumba vya maabara  inaonesha hadi  Desemba mwaka jana, vyumba 3,607 sawa
na asilimia 34 ya mahitaji ya vyumba 10,653 vya maabara nchini vilikuwa vimejengwa.
Aidha, vyumba 6,249 sawa na asilimia 59 ya mahitaji, vilikuwa vinaendelea kujengwa na asilimia saba vilikuwa havijaanza kujengwa.    
Wakati huo huo Pinda alisema bajeti ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura ni Sh bilioni 218 na ya Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, ni Sh bilioni 268. 
“Naelewa kwamba changamoto kubwa ni upatikanaji wa fedha hizi kwa muda muafaka. Hata hivyo, kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha kwamba fedha zinapatikana na kazi hii muhimu inafanyika kama ilivyopangwa,” alisema.  
Kuhusu Katiba Inayopendekezwa, Waziri Mkuu alitoa mwito kwa wakuu wa mikoa wote nchini, kuhakikisha wanasimamia kikamilifu usambazaji wa nakala zake.
Aidha ametaka wananchi wahimizwe kusoma Katiba hiyo, ili washiriki kikamilifu katika upigaji kura ya maoni utakaofanyika Aprili 30 mwaka huu.

No comments: