Serikali imesema Tume ya Utumishi wa
Walimu itaanza kazi Julai mwaka huu na
kuhudumia walimu katika masuala mbalimbali huku muundo wa utumishi wa tume hiyo
umehusisha ngazi za chini na juu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti
ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani alisema serikali imekubali kuanzisha tume
hiyo ya kuhudumia walimu nchini ili kuepuka walimu kuhudumiwa na wizara
mbalimbali.
Alisema tume hiyo itaanza rasmi mwezi huo
na kuingizwa kwenye bajeti ijayo, huku madeni ya walimu ya mishahara yakiwa
ni yaliyohakikiwa Sh bilioni sita na
ambayo hayajahakikiwa ni Sh bilioni
tatu.
Alisema ili kukabiliana na madeni ya
walimu, sasa serikali imeagiza taasisi zote ziweke kipaumbele katika malipo ya
likizo iwe kulipwa mapema kama mishahara.
Awali, Kamati ya Huduma za Jamii ilitaka
walimu nchini kusajiliwa ikiwa ni pamoja na wanaofanya kazi katika shule
binafsi ili kuwatambua walimu na kuweka
kiwango cha msingi cha kutoa huduma kwa walimu nchini kwa kuitumia Tume ya
Utumishi wa Walimu.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Margaret Sitta alisema kamati inapongeza kusudio la
serikali kuanzisha Tume ya Utumishi wa Walimu nchini katika mwaka wa fedha
2015/16.
Alisema kamati inashauri tume hiyo
kuanzishwa haraka ili kukabiliana na adha zinazowakabili walimu nchini na
kurejesha hadhi ya taaluma ya ualimu nchini.
No comments:
Post a Comment