DEREVA BODABODA ATUHUMIWA KULAWITI CHEKECHEA KIBAHA

Dereva bodaboda Ismail Lucas (16), mkazi wa Kwa Mathias wilayani Kibaha mkoani Pwani, anatuhumiwa kumlawiti mtoto  ambaye ni mwanafunzi wa Chekechea.

Mama wa mtoto huyo (jina limehifadhiwa) alisema kuwa kutokana na tukio hilo, mwanawe (jina limehifadhiwa) alijeruhiwa vibaya.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea saa 3:00 asubuhi eneo la Tanita wakati mtoto huyo alipokuwa akitokea dukani akiwa ameongozana na mwenzake, mtoto wa mama yake mkubwa mwenye umri wa miaka saba, ambaye alikuwa amewaagiza mkate.
“Mama yake mkubwa aliwatuma dukani Kwa Mrisho ambapo walinunua mkate na walipokuwa wakirudi, walikutana na mtuhumiwa ambaye alimrubuni mwanangu kuwa ameangusha chenji  iliyorudi dukani hivyo aende akampe,” alisema.
Alisema kuwa mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa na pikipiki, alimchukua na kumpeleka kwenye vichaka ambavyo viko jirani na barabara huku mwenzake akiwa analia kuomba msaada.
“Alikwenda naye huko vichakani na kumfanyia vitendo hivyo,  mama mmoja Clara Edwin alikuwa akipita hapo na alipomwona mtoto aliyekuwa akilia  alimwuliza imekuwaje, akamwambia mwenzangu kachukuliwa na mtu asiyemfahamu na kuelekea eneo la tukio, ndipo mtuhumiwa alipokimbia na kuacha pikipiki yake,” alisema.
Alisema kuwa yeye hakuwepo nyumbani, lakini alijulishwa kuwa mwanawe kafanyiwa mchezo huo, ambapo alipomwona mwanawe akiwa kwenye hali ile, alipoteza fahamu.
“Majirani walinisaidia baada ya muda nilizinduka na kumpeleka mtoto kituo cha Polisi cha Kwa Mathias na baadaye Hospitali ya Mkoa ya Tumbi kwa ajili ya matibabu ambapo hadi sasa anaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu,” alisema.
Kwa upande wake, Clara ambaye ndiye aliyemuokoa mtoto huyo, alisema yeye baada ya kwenda kule vichakani mtuhumiwa alikimbia kusikojulikana na wasamaria  waliipeleka pikipiki hiyo kwenye kijiwe anachofanyia kazi na ndipo walipobaini kuwa ni ya Lucas.
“Wasamaria wema wakishirikiana na madereva bodaboda wenzake, walifika nyumbani kwao na kumkuta mlezi wake ambapo walimwambia asimruhusu kuondoka hadi polisi watakapofika, ambapo walimchukua na kumpeleka kituoni,” alisema.
Akithibitisha kutokea tukio hilo,  Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei (pichani juu) alisema mtuhumiwa huyo anashikiliwa na atafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika.

No comments: