WAJIFUNGUA KWA VIBATARI MIAKA MITANO MASASI

Wajawazito wakazi wa kata za Sululu na  Matawale katika Halmashauri ya  Mji wa Masasi mkoani Mtwara, wamekuwa wanajifungua kwa kutumia vibatari  muda wa usiku zaidi ya miaka mitano sasa.


Diwani wa  Kata ya Sululu, Peter Mrope alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi. 
Alisema kuwa hali ya zahanati sio nzuri na zaidi ya miaka mitano wakazi wake na kata ya jirani ya Matawale, wanapougua au kujifungua wakati wa usiku, wauguzi na madaktari wanatumia vibatari ili wapate kumhudumia mgonjwa aliyefika muda huo.
Alisema zahanati hiyo iliyopo kijiji cha  Makalani, haina huduma za umeme au nishati ya jua, kiasi  huduma za afya kuzorota.
Mrope alisema baadhi ya wauguzi na watumishi  hawaipendi zahanati hiyo, kutokana miundombinu yake sio rafiki kwa watumishi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Masasi, Andrew Mtumisha alikiri kuwapo tatizo la ukosefu wa huduma ya umeme, linalosababisha wajawazito na wagonjwa wa magonjwa mbalimbali kutibiwa kwa kutumia vibatari katika zahanati ya Sululu.
Alisema tatizo hilo ni la muda mrefu. Alisema hakuna miundombinu ya umeme tangu  zahanati ikiwa katika Halmashauri ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.
Alisema  baada ya kugawa  maeneo ya mipaka na utawala kati ya Halmashauri  ya Mji na Halmashauri ya wilaya, kata ya Sululu ilipangwa kuwa ya Halmashauri ya Mji wa Masasi  mwaka 2012.
Alisema kipindi hicho, Mfuko wa Jimbo ambao uko chini ya Mbunge wa jimbo ulishaanza, lakini zahanati hiyo haijapata nishati ya jua ili kuondoa  tatizo la wagonjwa kujifungua kwa kutumia vibatari.
Alisema ofisi ya Mbunge na Uongozi wa Mfuko wa Jimbo, unapaswa kukagua maendeleo ya zahanati hiyo  na kuweza kubaini tatizo hilo.
Alisema kikao cha Baraza la Madiwani cha Januari 30, mwaka huu kiliagiza Ofisi ya Mkurugenzi kununua na kuweka umeme wa jua  kwa muda wa mwezi mmoja.
Mkurugenzi wa  Mji wa Masasi, Fortunatus Kaguro alikiri kupewa maazimio ya kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kununua nishati ya jua.

No comments: