Mlipuko wa kipindupindu ulioukumba mkoa
wa Kigoma, umesababisha vifo vya watu watano, huku wengine zaidi ya 170
wakilazwa hospitalini.
Hayo yalithibitishwa mjini hapa na
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Leonard Subi (pichani) akisema Manispaa ya Kigoma/Ujiji
imeathirika kwa kiasi kikubwa na ugonjwa huo, na kwamba tayari hatua mbalimbali
zimechukuliwa kukabiliana na hali hiyo.
Alisema tangu Januari mwaka huu,
ugonjwa huo ulioanza kuripotiwa kwenye wilaya ya Kasulu na Manispaa ya
Kigoma/Ujiji, watu 175 walikuwa wamekumbwa na ugonjwa huo katika Manispaa ya
Kigoma/Ujiji huku Kasulu ikiwa na wagonjwa wanane.
Alisema kwa Manispaa ya Kigoma/Ujiji,
eneo lililoathiriwa ni Kata ya Kibirizi ambako sehemu kubwa ya wagonjwa
waliougua na kufariki walitoka huko na kwamba tayari kambi ya wagonjwa wa
kipindupindu imefunguliwa kwenye kituo cha afya cha Gungu, Manispaa ya
Kigoma/Ujiji.
Akizungumzia hali hiyo, Mganga Mkuu wa
Manispaa ya Kigoma/Ujiji, John Maginga alisema hatua za kudhibiti ugonjwa huo
zimeshachukuliwa, ikiwemo kuvifunga baadhi ya visima ambavyo vimegunduliwa kuwa
na vimelea vya ugonjwa huo.
Hata hivyo, alisema kufungwa kwa visima
vitatu vya Senzia, Kibore na Msulula B ambavyo viligundulika kuwa na vimelea
vya ugonjwa wa kipindupindu hakukubaliwa na wananchi wa eneo hilo la Kibirizi,
kwani wananchi waliendelea kuvitumia visima hivyo kwa siri usiku, jambo ambalo
limelilazimu mamlaka kuweka ulinzi ambao unavilinda visima hivyo kwa masaa 24.
Mganga huyo wa Manispaa alitaja hatua
nyingine ambazo zimechukuliwa kuwa ni pamoja na kufunga shughuli zote za uuzaji
vyakula magengeni (mama ntilie), kutoa elimu kwa njia ya magari, kusambaza
vipeperushi kwenye maeneo ya mkusanyiko, ikiwemo kwenye nyumba za ibada kwenye
masoko na vituo vya magari.
Hofu zaidi iko katika vyombo vya usafiri,
kwani Kigoma ni moja ya mikoa inayoingiliana na mikoa mingi nchini, hasa
kutokana na usafiri wa treni unaoanzia Dar es Salaam na kupitia mikoa ya
Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora ambako baadhi ya mabehewa hugawanya na kwenda
Mwanza na Shinyanga, huku mengine yakienda Mpanda mkoani Katavi.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa
Manispaa ya Kigoma - Ujiji wamelalamikia kukithiri kwa uchafu katika manispaa
hiyo kunakotokana na kuzagaa kwa uchafu kufuatia ofisi ya afya ya Manispaa hiyo
kushindwa kuzoa taka zinazokusanywa kwenye vizimba na mitaani.
No comments:
Post a Comment