Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) unakabiliwa
na changamoto ya kifedha katika ujenzi wa miundombinu, kutokana na ongezeko la mahitaji ya fedha za
kuukamilisha.
Bunge lilielezwa kwamba ongezeko la mahitaji ya fedha za
kukamilisha mradi huo ni Sh bilioni 64.7, ambazo kati yake Sh bilioni 20.6 ni
ongezeko la mishahara na Sh bilioni 44.1 ni ongezeko la kazi na madai mengine.
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, Dk Athuman Mfutakamba alisema hayo jana wakati akiwasilisha taarifa ya
mwaka ya kamati kuanzia Januari 2014 hadi 2015.
Kamati hiyo imeishauri
serikali kufanya jitihada za makusudi, kuhakikisha mradi unaendelea kutekelezwa
kama ilivyopangwa na fedha yote inayohitajika kukamilisha hatua mbalimbali za
mradi, zinatengwa na kupelekwa hatua zikamilike kwa wakati.
Kwa mujibu wa Mfutakamba, inadaiwa ongezeko hilo limefanya
mkandarasi kutoonesha utayari wa kuanza kazi katika barabara ya Msimbazi kwa
hofu ya kutokuwepo kwa fedha za kumlipa.
Changamoto nyingine ambayo wabunge walielezwa kwamba inakabili
mradi, ni uharibifu wa miundombinu ambao baadhi ya wananchi na wafanyabiashara
ndogo huvamia maeneo ya ujenzi yanayoendelea.
Vile vile kumekuwapo tabia ya wizi wa samani za barabara, mifuniko
ya maji ya mvua, maji taka na huduma nyingine.
No comments:
Post a Comment